Saturday, 30 July 2016

AINA ZA NDOA NA HUKUMU ZAKE

Unknown

Aina Za Ndoa Na Hukumu Zake

Katika makala hii fupi inshaAllaah tutajaribu kuzitambulisha aina za ndoa na kuweza kuzijua hukumu zake kisheria pamoja na maelezo kwa ufupi.
Ndoa ni miongoni mwa alama na miujiza yake Allaah (Subhaanahu Wata’ala) na ina dalili ya kuthibitika kwake katika Qur’aan na katika Sunnah.
Katika Qur’aan
Suuratu Nnisaa/3
 وَإِنْ خِفْتُمْ أَلاَّ تُقْسِطُواْ فِي الْيَتَامَى فَانكِحُواْ مَا طَابَ لَكُم مِّنَ النِّسَاء مَثْنَى وَثُلاَثَ وَرُبَاعَ فَإِنْ خِفْتُمْ أَلاَّ تَعْدِلُواْ فَوَاحِدَةً أَوْ مَا مَلَكَتْ أَيْمَانُكُم
“Na ikiwa mnaogopa kuwa hamtowafanyia mayatima uadilifu, basi oeni mnaowapenda katika wanawake, wawili au watatu au wanne. Na mkiogopa kuwa hamwezi kufanya uadilifu, basi mmoja tu, au wale ambao mikono yenu ya kulia imewamiliki.”

Suuratu Nnuur/32
وَأَنكِحُوا الْأَيَامَى مِنكُمْ وَالصَّالِحِينَ مِنْ عِبَادِكُمْ وَإِمَائِكُم
“Na waozeni wajane miongoni mwenu na wema katika watumwa wenu na wajakazi wenu.”


Katika Sunnah
يامعشر الشباب ، من استطاع منكم الباءة فليتزوج فإنه أغض للبصر  وأحصن للفرج ، ومن لم يستطع فعليه  بالصوم فإنه له وجاء
 أخرجه البخاري
“Enyi vijana! Mwenye uwezo wa kuisimamia ndoa na aoe kwani huko ni kuweza kuinamisha macho na kuweza kuzikinga tupu na kama hamna uwezo basi ni juu yenu kufunga kwani huko ndiko kwenye kinga.” Al-Bukhaariy
Na pia:
النكاح من سنتي ، فمن لم يعمل بسنتي فليس مني
Ndoa ni miongoni mwa Sunnah zangu na mwenye kutenda kinyume na Sunnah zangu hatokuwa pamoja na mimi. Ibn Maajah
Ili ndoa ikamilike hupaswa kutimiza nguzo, masharti pamoja na adabu zake vinginevyo inaweza kuwa miongoni mwa ndoa zenye utata katika uhalali wake.
Ndoa, kwa mujibu wa Rai za Jamhuur Ulamaa (isipokuwa Abu Haniyfah), zimegawika kwenye sehemu kuu tatu zifuatazo:
1       Ndoa sahihi iliyokamilika
         Iliyotimiza nguzo na masharti ya kusihi kwake na kuweza kutekelezwa.
2       Ndoa Sahihi isiyokamilika
         Iliyotimiza nguzo na masharti ya kusihi kwake lakini imeshindwa kutekelezwa.
3       Ndoa batili au fasidi
         Iliyokosekana moja ya nguzo au masharti ya kusihi kwake.



Yanayopaswa kuwepo wakati wa kufungwa ndoa (Aqdi)
Ni yafuatayo
1       Kuwepo mke na mume (ambao wataweza kuisimamia ndoa na kutokuwepo vizuizi vya kuwazuia                    kuoana)-miongoni mwa masharti ya ndoa.
2       Ijaabu (tamko la kuoa au kuozesha) na Qabuul (tamko la kukubali) – miongoni mwa nguzo za ndoa
3       Awepo walii -miongoni mwa masharti ya ndoa
4       Wawepo Mashahidi – miongoni mwa masharti ya ndoa
Yanayopaswa kuzingatiwa
Ni yafuatayo
  • Asiwe mmoja wa wanandoa ana vizuizi vya kuwafanya wasioane ikiwa ni vya muda au vya kudumu.
  • Mkataba wa ndoa uwe wa kudumu usiwekewe muda maalum.
  • Ridhaa, chaguo na uamuzi uwe ni wa wanandoa kusiwepo kulazimishana.
  • Wasiwe wanandoa katika hali ya kuhirimia kwa ajili ya Hajj au ’Umrah.
  • Yawepo mahari.
  • Wajulikane wanaooa au kuolewa.
  • Kusiwepo mbinu za kutoitangaza ndoa na kuificha.

Ndoa batili au fasidi
1NDOA FASIDI/ BATILIIliyofisidika kwa kukosekana moja katika nguzo, masharti ya msingi ya kufungika ndoa.Ndoa hutakiwa ikamilike mambo yake yote zikiwemo nguzo masharti ya kusihi kwake ili iweze kuwa na uhalali kisheria.Haijuzu
2NDOA WAKATI WA IHRAAMUKuoa/kuolewa wakati mmeshahirimia ima kwa ibadah ya Hajj au ‘Umrah.Kuwepo katika hali ya Ihraamu ni moja katika mambo yanayomzuia mke/mume kufanya tendo la ndoa na kuoa au kuwakilishwa ndoa pia ni mambo yasiyofanywa kwa aliye kwenye Ihraamu.Haijuzu
3NDOA BILA YA WALIIKufungwa ndoa kwa kuwepo mke na mume pamoja na mashahidi lakini Walii amekosekana.Ndoa haikamiliki bila ya kuwepo kwa Walii na ni mojawapo ya nguzo za ndoa. Walii ni mwenye haki ya kumuozesha na kusimamia ndoa kwa niaba ya binti.Haijuzu kwa mujibu wa Jamhuur Ulamaa na inajuzu kwa mwanamke aliye baleghe kujiozesha kwa mujibu wa rai ya Abu Haniyfah.
4NDOA YA “WALII” ASIYEKUWA NA SIFAKufungwa ndoa kwa kutimizwa masharti yote isipokuwa walii ni mama wa binti kwa kukosekana baba na mfano wake.Moja katika masharti ya kusihi ndoa ni kuwepo walii mwanamme. Kisheria walii ni mwanamme na mwanamke si miongoni mwa walii wa binti.Haijuzu
5NDOA BILA YA KUWEPO MASHAHIDIKufungwa ndoa wakiwepo mke na mume na walii bila ya kuwepo shahidi kama ilivyo ndoa ya Mut’ah au ndoa ya siriNi moja katika masharti ya kusihi ndoa kwamba lazima ishuhudishwe na mashahidi ili kuondosha dhana ya kuwepo ndoa za siri na kuondosha tuhuma na dhana.Haijuzu


Ndoa zenye utata katika kujuzu kwake
 NDOAMAELEZOSABABUHUKUMU
1NDOA YA MUT’AH (MUDA MAALUM)Hufungwa kwa muda maalum japo masaa mawili, bila mashahidi wala walii, ambapo wanandoa kuwa na haki kama wameoana.Imewekewa muda maalum na hakuna kurithiana wala kutalikiana.Haijuzu
2NDOA YA MHALILI (ALIYEACHIKA TALAKA TATU)Kuolewa mke aliyeachika talaka tatu si kwa lengo la ndoa bali kwa lengo la kuipinda sheria ili ahalalishiwe mume wa mwanzo.Mume anataka kurudiana na mkewe ambaye kamuacha talaka tatu na hivyo kumtafuta mume mwengine amuoe mkewe kwa makubaliano lakini pasipatikane tendo la ndoa kisha amuache.
Kisheria atatakiwa aolewe na mume mwengine ndoa halisi na papatikane tendo la ndoa.
Haijuzu
3NDOA ZAIDI YA WAKE WANEMume kuoa wake zaidi ya wane kwa wakati mmoja waliokubalika kisheria.Ruhusa na mipaka tuliyowekewa na sheria ni kuwa na wake wane tu kwa wakati mmoja. (Na hata kama mke  ameachika talaka rejea  na yupo katika eda basi uharamu upo pale pale).Haijuzu
4KUOLEWA NA MUME ZAIDI YA MMOJA  WAKATI MMOJAMke kuolewa na mume zaidi ya mmoja kwa wakati mmoja yaani kuwa na waume wawili na kuendelea.Sheria inakataza mke kuolewa na waume wengi kwa wakati mmoja kwani ni kinyume na fitrah- maumbile ya asli (Uislamu).Haijuzu
5NDOA KWENYE EDAKumuoa au hata kumposa mke aliyeachika na bado yupo katika eda na hakuwa mke wake kabla.Kuwepo kwenye eda ya aina yoyote kwa mke ni kizuizi kinachomfunga kutoweza kuolewa mpaka imalizike isipokuwa kwa mtalaka wake tu kama mke aliyeachika talaka rejea.Haijuzu
6NDOA KWENYE UJA UZITO KWA MWANAMKE AMBAYE HAJAPATA KUOLEWA KABLAKwa mwanamke ambaye hajaolewa akazini na kupatikana ujauzito na kutaka kuolewa katika hali hii. Ndoa hizi hufanyika pale mambo yameshaharibika na kutaka kusitirianaUjauzito utakuwa na hukumu sawa kama mwanamke aliye katika eda (Ahmad na Abu Haniyfah). Uja uzito hautokuwa na hukumu sawa kama mwanamke aliye katika eda (Maalik na ash-Shafi’iy).Haijuzu kwa rai ya Ahmad na Abu Haniyfah
Inajuzu kwa rai ya Maalik na ash-Shafi’iy ila tu hatopaswa kustarehe naye mpaka ajifungue.
7NDOA KWENYE UJA UZITO KWA ALIYEACHIKAMke aliyeachika na ni mja mzito na kutaka kuolewa na mume mwengine asiyekuwa mtaliki wake.Mke aliyeachika katika uja uzito yupo katika Eda na humalizika atakapojifungua na kumaliza muda wake wa Nifasi. Kisheria Eda  inamfunga mke  kuolewa mpaka imalizike.Haijuzu
8NDOA KWA ASIYEKUWA MUISLAMU WALA HAKUTEREMSHIWA KITABU

Kuoa washirikina  na makafiri ambao si miongoni mwa walioteremshiwa vitabu kama mayahudi na manasara.Moja katika masharti ya kusihi ndoa ni Uislamu. Hivyo kuoa asiyekuwa Muislamu huifanya ndoa kuwa fasidi.Haijuzu
9NDOA KWA ASIYE MUISLAMU LAKINI NI MIONGONI MWA WALIOTEREMSHIWA KITABUWalioteremshiwa vitabu miongoni mwa mayahudi na manasara na wanaowafuata katika mila zao.Uislamu ni moja ya masharti ya kusihi ndoa ila kwa mujibu wa aya za Qur’aan wameruhusika kuolewa.Inajuzu ingawa ni Makruuh – haipendezi
10KUOLEWA MUISLAMU NA ASIYEKUWA MUISLAMUMwanamke wa Kiislamu kuolewa na kafiri, mwenye kumshirikisha Allaah pamoja na mayahudi na manasara.Ndoa hulazimisha utiifu wa mke kwa  mumewe na hivyo kuwepo khofu ya kuweza kuathirika na kubadilisha dini na watoto kufuata dini ya baba.

Haijuzu
11KUOA/KUOLEWA NA ALIYERTADIMwanamme au mwanamke aliyekuwa Muislamu kisha akaamua kurtadi – kutoka katika dini.Kwa kukosekana sharti la msingi la Uislamu na hata kama atakuwa amekwenda katika dini ya walioteremshiwa vitabu.Haijuzu
12KUMUOA BINTI ULIYEZAA NJE YA NDOAMwanamme kuoa binti aliyezaa baada kutembea (kuzini) na mama yake nje ya ndoa.Huyu ni mtoto wake kwani ni mbegu zake ila tu atakosa baadhi ya haki za kimsingi kwa kuzaliwa nje ya ndoa.Haijuzu
13KUOA BINTI WA KAMBO AMBAYE MLIWAHI KUWA NA MAHUSIANO HARAMU NA MAMA YAKEKuoa binti wa kambo ambaye mliwahi kuwa na uhusiano haramu (zinaa) na mama yake kabla. Si binti aliyezaa nje ya ndoa bali ni binti wa mama.Kutokana na kupatikana tendo la haramu la zinaa Maulamaa wametofautiana katika tendo hili (zinaa) je llitaweza kuharamisha halali (ndoa)? Na kuna Qaaidah-“Haramu haiwezi kuifanya halali nyengine kuwa haramu”. Kuna Qaaidah nyengine “tendo la haramu huharamisha halali”.

Inajuzu kwa rai ya ash-Shaafi’iy na Maalik kwa sababu ya kutokuwepo dalili bayana kuharamisha. Haijuzu kwa rai ya Abu Haniyfah na Ahmad bin Hanbal kwa sababu ya kuwepo tendo la haramu zinaa.
14KUOA BINTI WA KAMBO AMBAYE MLIWAHI KUWA NA MAHUSIANO HALALI NA MAMA YAKEKuoa binti wa kambo ambaye kuliwahi kuwepo mahusiano ya halali (ndoa) na mama yake mzazi na binti huyu si miongoni mwa watoto wa mume.na Qaaidah – msingi wa kisheria yakipatikana maingiliano kwa mama huharamisha (kuolewa) binti yake.

Haijuzu

15KUOA MAMA AMBAYE ULIWAHI KUOA BINTI YAKEKumuoa mama ambaye kabla mliwahi kuwa na uhusiano wa ndoa na binti yake.Haijuzu
16NDOA KWA WALIONYONYA ZIWA MOJAIkiwa watoto wa kike na wa kiume wametokezea kunyonya ziwa moja kwa mama mmoja na wakataka kuoana.Moja katika mambo yanayoharamisha ndoa ni kuoa /kuolewa na mliyenyonya ziwa moja kwani kitendo hiki tayari kisheria kimeshaunda udugu baina yao.Haijuzu
17NDOA YA KUBADILISHANA (SHIGHAAR)Mwanamme kumuozesha binti/dada yake kwa mwanamme mwengine ambaye naye atamuozesha binti/dada yake kwa mwanamme wa mwanzo kwa mabadilishano.Ndoa hizi hufanyika pasi na kutajwa mahari kwani mahari ya kila mmoja ni kumkubalia mwengine kuoa kwake “nipe nikupe” na pasi na kupatikana ridhaa ya upande mwengine.Rai yenye nguvu haijuzu kwa kufanyika kinyume na misingi ya ndoa ya Kiislamu.
18NDOA YA BOMANINdoa zinazofungishwa na wakuu wa wilaya au kwenye ofisi za wasajili wa ndoa serikalini.Hufanyika bila ya kutekelezwa masharti ya kimsingi katika sheria za ndoa za Kiislamu kwani si lazima kuwepo mashahidi au kuwa wanandoa ni wa dini moja.Haijuzu.

Ikiwa taratibu za nchi zinahitaji kufungwa ndoa hii itawajibika kwanza kufungwa ndoa ya Kiislamu.
19NDOA YA MISYAARMwanamke hukubali kuolewa huku akisamehe baadhi ya haki zake za kimsingi katika ndoa kama mahari, huduma na makaazi au hata katika kugawana siku (kwa wake wenza).Ndoa hizi hufanyika sana katika Bara Arabu hasa kutokana na ughali wa mahari na hivyo mke katika kutafuta stara huzisamehe baadhi ya haki zake.
Na pia kama wenye kuoa Afrika huku wakiwa na mke mwengine na hivyo mke wa Afrika kusamehe baadhi ya haki zake kama za kugawana siku na nyenginezo kwa kuwa anapata huduma nyengine kama pesa na kadhalika.
Itajuzu ikiwa  imetimiza masharti ya kimsingi – Haitojuzu ikiwa haitotimiza masharti ya kimsingi kama kufanyika ndoa ya Misyaar bila ya Walii.
20NDOA YA MISFAARHufungwa kwa muda maalum kama wakati wa mapumziko au kwa wafanyakazi, wanafunzi ambao wako mbali na miji au nchi zao humalizika baada ya kurudi sehemu zao walikotokaKimsingi ndoa yoyote itakayowekewa mkataba/muda maalum kumalizika kwake haikubaliki kisheria kama ilivyo Mut’ah. Mfano wanandoa wamekubaliana kuoana wakiwa Uingereza tu lakini wakirudi walipotoka ndoa imemalizika hata bila ya talaka.Haijuzu kwa rai ya Jamhuur
Licha ya kutimiza masharti yote ya kimsingi ila kwa kuwepo muwafaka wa kumalizika kwake ambao ni kinyume na taratibu za ndoa ya Kiislamu.
Itajuzu kwa rai ya Abu Haniyfah ikiwa sharti la kumalizika halitozingatiwa kwani ni sharti batili.

21KUOA MWANAMKE ALIYEPOSWA KABLAKuvunja uchumba uliopo na kuposa kisha kumuoa binti ambaye tayari ameshachumbiwa.Kwenda kuposa mwanamke aliyeposwa ni haramu kisheria. Kwa mujibu wa Hadithi za Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam. Ikiwa atakayeposa anajua taarifa za kuposwa kwa binti kabla basi
mtendaji ni mwenye madhambi na dhimma kwa kukiuka makatazo.
Kama hakujua na kufahamu baadae basi uharamu upo pale pale
Ndoa itajuzu kwa mujibu wa rai ya Jamhuur Ulamaa kwa sababu kilicho haramu kilitokea kabla ya kufungwa na si katika ndoa kwani khutba si miongoni mwa mwa masharti ya kusihi ndoa.

Haijuzu kwa mujibu wa Maalik na kama ndoa itafanyika itabidi ibatilishwe

22NDOA YA KUJIFICHA  “SIRI”Kuoana kwa kukamilisha nguzo na masharti yote ya ndoa ila tu wanandoa na mashahidi kutakiwa kutoitangaza na kuidhihirsha.Ikiwa ndoa hii itakamilika katika idara zote ila kilichokosekana ni mashahidi tu kuitangaza ndoa. Kama kuoa mke wa zaidi ya mmoja bila ya kumtaarifu mke/wake/watu wengine.Inajuzu kwa sababu ndoa imekamilika kuwepo mashahidi kumeifanya si siri tena, imeshatangazwa. Ila ni jambo lisilopendeza kisheria (makruuh)
24KUOA KWA  NIA YA KUACHAMume kuoa na katika mkataba wa ndoa akashurutisha kwamba atamuacha mke katika muda fulani au bila ya kushurutisha lakini tayari ameshaweka nia katika nafsi yake ya kuacha.Kimsingi ndoa yoyote itakayowekewa mkataba/muda maalum kumalizika kwake haikubaliki kisheria ikiwa imeshurutishwa au kuwekwa nia kwani inakuwa ndoa ya muda maalum. Na kuwepo ndani yake hadaa na udanganyifu.Haijuzu kwa rai ya Jamhuur kwa sababu ya kuwekewa muda wa kumalizika na udanganyifu.

Itaweza kujuzu kwa rai ya Abu Haniyfah ikiwa shurti litabatilishwa na kutenguliwa



Ni muhimu kwa kila Muislamu kuzifahamu vyema aina hizi na kuhakikisha ndoa yake imefungwa katika misingi na taratibu zilizo sahihi. Na kama ni miongoni mwa watakaosimamia au kuwakilisha katika ndoa wazingatie maelezo haya ili waweze kuwa na uelevu katika mwenendo mzima wa ndoa kuepuka matatizo na kuepukana na ndoa zenye utata.
Pia kuwepo tayari kuusimamia ukweli na haki pale ambapo ndoa iliyofungwa ilifungwa katika misingi isiyokuwa sahihi au baadhi ya taratibu zake kukiukwa.
Ikiwa ndoa ni moja katika alama zake Allah Subhaanahu Wata’ala na miujiza yake hatuna budi Waislamu kuhakikisha kuzithibitisha alama hizi kwa kuifunga katika misingi na taratibu sahihi za kisheria.
Na Allah Ndiye Ajuaye zaidi

WAJIBU WA MUME KWA MKE

Unknown

Wajibu wa mume kwa mkewe

"MUME wangu mkali kweli, akirudi nyumbani hakuna mazungumzo, huzungumza anapotaka yeye. Kitu kidogo kafoka, ukiimuliza hakujibu, anapokuuliza yeye anakutaka ujibu haraka, haya ndio maisha tunayoishi katika nyumba yetu", ameeleza mama Zumaraa alipokuwa akiongea na mke wa rafiki wa mumewe katika masukano ya nywele maeneo ya Hailallah (Ilala) jijini.

Naye mama Tadei wa mikocheni ana haya ya kusema "mume wangu hurudi nyumbani baada ya kutoka kilabuni, akifika anataka akute chakula kikiwa tayari mezani, hana mazungumzo na mimi wala watoto, asubuhi akiamka anataka chai iwe tayari mezani, wenzenu nimekuwa mpishi sio mke tena"

Akina mama hawa ni baadhi tu ya wanawake wengi wenye malalamiko kama hayo dhidi ya waume wanaopuuza au kutokujua wajibu kwa wake zao.
Katika jamii nyingi mwanamke hufanywa kama mtumishi au mtumwa anayetakiwa kutii kinyonge amri za bwana wake(mumewe). Katika baadhi ya jamii hizo, mwanamke anaangaliwa kama kifaa kingine cha nyumbani.

Kwa upande mwingine, mwanaume hana wajibu atakiwao kuutekeleza kwa mkewe, bali mkewe ndiye tu aliyelazimika kuwajibika kwa bwana wake. Familia na jamii nyingi zinauona uhusiano wa mume na mke ni kama ule wa "Bwana" na "Mtumwa" wake.
Katika Uislamu uhusiano wa mume na mke ni ule wa mtu na mwenzie au mtu na mpenzi wake. Kwa hiyo mke katika Uislamu si mpishi au mfanya usafi wa nyumba bali ni mwenza wa maridhiano ya kimapenzi kati yake na mumewe. Uhusiano huu wa mume na mke ndio lengo kuu la ndoa. Kama tunavyojifunza katika Qur'an:

Na katika ishara zake ni kuwa amekuumbieni wake zenu katika jinsi yenu ili mpate utulivu kwao, naye amejaalia mapenzi na huruma baina yenu... (30:21).

Mapenzi na huruma vitakuwepo tu endapo tangu awali walichaguana kwa dhati moyo iliyotokana na kila mmoja kupenda aishi na huyo mwenzi wake kama mume na mke ambapo kila mmoja atalazimika kutekeleza wajibu wake kwa kadiri ya uwezo wake na kwa upendo wa huruma.
Katika Uislamu mwanaume anawajibika kwa mkewe au kumpa mkewe haki zifuatazo:
Huduma zote za ikiwa ni pamoja na chakula, nguo na makazi kwa kadri ya uwezo wake.
Mwanaume hatarajiwi kumgharamia mkewe zaidi ya uwezo wake:

Mwenye wasaa agharamike kadri ya wasaa wake, na yule ambaye amepungukiwa riziki yake, atoe katika kile alichopewa na Mwenyezi Mungu; Mwenyezi Mungu hamkalifishi mtu yeyote ila kwa kadri ya alichompa. Atajaalia Mwenyezi Mungu baada ya dhiki faraja. (65:7).

Kumtendea, wema, kumhurumia na kumpenda:

Na kaeni kwa wema; na kama mkiwachukia basi (miswawache) kwani huenda mkachukia kitu, na Mwenyezi Mungu ametia kheri nyingi ndani yake. (4:19).

Katika hadithi iliyosimuliwa na Aysha (r.a.), Mtume (s.a.w.) amesema:

Mbora miongoni mwenu ni yule aliye mbora katika (kuwatendea wema) familia yake na ni mbora wenu katika familia yangu... (Ibn Majah).
Pia Abu Hurairah (r.a.) kasimulia kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu amesema:
Muislamu aliyekamilika kweli kweli miongoni mwenu katika imani ni yule aliye mbora wao katika tabia, na wabora katika nyinyi ni wale ambao ni wabora kwa wake zao. ('Tirmiz, Abu Daud).

Katika Qur'an na hadithi wanaume wamesisitizwa sana kuwafanyia wema wake zao, na kuwaonesha upendo na huruma.

Ili kuzidisha mapenzi, inapendekezwa kwa mwanamume kuwa, pamoja na kumpatia mkewe mahitaji muhimu, mara kwa mara amletee zawadi kila atakapopata wasaa.

Vile vile, mume ameshauriwa mara kwa mara apate muda wa kuongea, kufurahi na kufanya matembezi na mkewe. Tunajifunza katika hadithi nyingi kuwa Mtume (s.a.w.) alikuwa akifurahi na wakeze.

Kujizuia na kumchukia mkewe

Chuki ni kinyume cha upendo. Kumchukia mke ni ndoa kubwa katika nyumba, hivyo mwanamume anatakiwa ajitahidi kujiepusha na kumchukia mkewe, kwa kuyabeza maudhi madogo madogo yasiyo ya msingi kama Mtume (s.a.w.) anavyotushauri katika hadithi ifuatayo:

Abu Hurairah ameeleza kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu amesema: "Mwanamume aliyeamini na asimchukie mwanamke aliyeamini. Kama anachukia kipengele kimoja cha tabia yake, atafurahishwa na kipengele kingine kizuri katika tabia yake. (Muslim).

Hadithi hii inasisitiza kuvumiliana kwa kuyaangalia mazuri ya mtu na kuyafumbia macho mabaya yake. Kwani ni muhali mwanaadamu kukosa mabaya, angalau kidogo.

Kupigana na kuwa mkali kama pili pili

Mwanaume haruhusiwi kumpiga mkewe kwa makosa madogo madogo. Haruhusiwi kumpiga fimbo au kofi la usoni bali anaruhusiwa kumpiga kwa nguo au mti wa mswaki kiasi cha kumpa onyo. Kabla ya kufikia hatua hii ya kuwapeana maonyo Qur'an inatuelekeza tuwahame katika vitanda mpaka watakapo jirekebisha (4:34).
Mtume (s.a.w.) ametushauri katika hadithi mbali mbali kuwa, tuwe na subira na ustahamilivu juu ya wake zetu, kama tunavyojifunza katika hadithi ifuatayo:
Ilyas bin Abdullah ameeleza kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu amesema: "Msiwapige vijakazi vya Mwenyezi Mungu (s.w.) (wanawake). Kisha Umar alikuja kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu akasema: Wanawake wanawakalia (hawawajali) waume zao sasa. Kwa hivyo (Mtume) aliwaruhusu wawapige. (Kesho yake baada ya ruhusa hii) wanawake wengi wakawa wanaranda-randa katika mazingira ya nyumba ya Mtume wa Mwenyezi Mungu wakilalamika dhidi ya waume zao.
Mtume wa Mwenyezi Mungu akasema: "Wanawake wamerandaranda nyumbani kwa Muhammad wakilalamika dhidi ya waume zao. Wanaume hao sio wabora miongoni mwenu." (Abu Daud, Ibn Majah).
Hadithi hii inatuweka wazi kuwa, japo kupiga kunaruhusiwa, lakini kisiwe kipigo kikubwa cha kuumiza. Hata hicho kipigo hafifu si jambo linalopendeza mbele ya Mwenyezi Mungu (s.w.) na Mtume wake. Mtume (s.a.w.) ambaye ni kiigizo chetu, hatuoni popote alipothubutu kumnyoshea mkono, yeyote katika wake zake. Tunajifunza kuwa kutokana na ukorofi wa wakeze, aliwahi kuwahama kwa kipindi cha mwezi mmoja. Ili tuweze kuishi vizuri na wake zetu.

Kutunza siri za unyumba.

Ni jambo baya sana mbele ya Mwenyezi Mungu (s.w.) mtu kutoa siri za nyumbani kupeleka nje hasa zile zinazohusu unyumba. Utoaji wa siri za unyumba unaondoa uaminifu kati ya mke na mume, inaondoa upendo kati yao, na unatoa mwanya kwa maadui kuwaingilia na kuvunja nyumba yao.

Kuwa muadilifu

Mwanamume akiwa na mke zaidi ya mmoja, awe muadilifu na kuwagawia haki zao pasina upendeleo wowote. Ikitokea kuwa kuna kitu ambacho hakiwezekani kugawanyika itabidi wake zake wote waamue kwa pamoja kuwa nani kati yao apate kitu hicho kwa niaba ya wengine la sivyo itapigwa kura, na kitu hicho kitakuwa ni cha yule atakayeangukiwa na kura.

Mtume (s.a.w.) ambaye ni kiigizo chetu, alikuwa muadilifu mno na mwenye kugawa haki sawa kwa wake zake kama tunavyojifunza katika hadithi ifuatayo:
Aysha (r.a.) ameeleza kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu alikuwa akigawanya ngono kwa wake zake kwa usawa. Alikuwa akisema: "Ee Mwenyezi Mungu huu ndio mgawanyo wangu kulingana na uwezo wangu. Hivyo usinipatilize kwa kile ulicho na mamlaka nacho, ambacho mimi sina. (Tirmidh, Ahmed, Nisai).
Mtu kupendelea baadhi ya wakeze katika kuwapa haki zao, ni jambo baya mno, ambalo linaweza likawa ndio sababu ya mtu kuingia motoni kama tunavyojifunza katika hadithi ifuatayo:
Abu Hurairah ameeleza kuwa Mtume (s.a.w) amesema: Mtu mwenye wake wawili akawa anampendelea mmoja kati yao, atakuwa siku ya Kiyama na upande mmoja unaoning'inia chini. (Tirmidh, Abu Daud, Nisai).


Mwanaume akijitahidi kumpa mkewe haki zake na akawa muadilifu kwake, akajitahidi kuonesha mahaba kwake na akawa mvumilivu na mwenye subira juu ya udhaifu wake, kwa vyovyote vile atapendana na kushikamana vilivyo na mkewe endapo mkewe atakuwa ni Muumini na mcha-Mungu. 

Coprights @ 2016,