"MUME wangu mkali kweli, akirudi nyumbani hakuna mazungumzo, huzungumza anapotaka yeye. Kitu kidogo kafoka, ukiimuliza hakujibu, anapokuuliza yeye anakutaka ujibu haraka, haya ndio maisha tunayoishi katika nyumba yetu", ameeleza mama Zumaraa alipokuwa akiongea na mke wa rafiki wa mumewe katika masukano ya nywele maeneo ya Hailallah (Ilala) jijini.
Naye mama Tadei wa mikocheni ana haya ya kusema "mume wangu hurudi nyumbani baada ya kutoka kilabuni, akifika anataka akute chakula kikiwa tayari mezani, hana mazungumzo na mimi wala watoto, asubuhi akiamka anataka chai iwe tayari mezani, wenzenu nimekuwa mpishi sio mke tena"
Akina mama hawa ni baadhi tu ya wanawake wengi wenye malalamiko kama hayo dhidi ya waume wanaopuuza au kutokujua wajibu kwa wake zao.
Katika jamii nyingi mwanamke hufanywa kama mtumishi au mtumwa anayetakiwa kutii kinyonge amri za bwana wake(mumewe). Katika baadhi ya jamii hizo, mwanamke anaangaliwa kama kifaa kingine cha nyumbani.
Kwa upande mwingine, mwanaume hana wajibu atakiwao kuutekeleza kwa mkewe, bali mkewe ndiye tu aliyelazimika kuwajibika kwa bwana wake. Familia na jamii nyingi zinauona uhusiano wa mume na mke ni kama ule wa "Bwana" na "Mtumwa" wake.
Katika Uislamu uhusiano wa mume na mke ni ule wa mtu na mwenzie au mtu na mpenzi wake. Kwa hiyo mke katika Uislamu si mpishi au mfanya usafi wa nyumba bali ni mwenza wa maridhiano ya kimapenzi kati yake na mumewe. Uhusiano huu wa mume na mke ndio lengo kuu la ndoa. Kama tunavyojifunza katika Qur'an:
Na katika ishara zake ni kuwa amekuumbieni wake zenu katika jinsi yenu ili mpate utulivu kwao, naye amejaalia mapenzi na huruma baina yenu... (30:21).
Mapenzi na huruma vitakuwepo tu endapo tangu awali walichaguana kwa dhati moyo iliyotokana na kila mmoja kupenda aishi na huyo mwenzi wake kama mume na mke ambapo kila mmoja atalazimika kutekeleza wajibu wake kwa kadiri ya uwezo wake na kwa upendo wa huruma.
Katika Uislamu mwanaume anawajibika kwa mkewe au kumpa mkewe haki zifuatazo:
Huduma zote za ikiwa ni pamoja na chakula, nguo na makazi kwa kadri ya uwezo wake.
Mwanaume hatarajiwi kumgharamia mkewe zaidi ya uwezo wake:
Mwenye wasaa agharamike kadri ya wasaa wake, na yule ambaye amepungukiwa riziki yake, atoe katika kile alichopewa na Mwenyezi Mungu; Mwenyezi Mungu hamkalifishi mtu yeyote ila kwa kadri ya alichompa. Atajaalia Mwenyezi Mungu baada ya dhiki faraja. (65:7).
Kumtendea, wema, kumhurumia na kumpenda:
Na kaeni kwa wema; na kama mkiwachukia basi (miswawache) kwani huenda mkachukia kitu, na Mwenyezi Mungu ametia kheri nyingi ndani yake. (4:19).
Katika hadithi iliyosimuliwa na Aysha (r.a.), Mtume (s.a.w.) amesema:
Mbora miongoni mwenu ni yule aliye mbora katika (kuwatendea wema) familia yake na ni mbora wenu katika familia yangu... (Ibn Majah).
Pia Abu Hurairah (r.a.) kasimulia kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu amesema:
Muislamu aliyekamilika kweli kweli miongoni mwenu katika imani ni yule aliye mbora wao katika tabia, na wabora katika nyinyi ni wale ambao ni wabora kwa wake zao. ('Tirmiz, Abu Daud).
Katika Qur'an na hadithi wanaume wamesisitizwa sana kuwafanyia wema wake zao, na kuwaonesha upendo na huruma.
Ili kuzidisha mapenzi, inapendekezwa kwa mwanamume kuwa, pamoja na kumpatia mkewe mahitaji muhimu, mara kwa mara amletee zawadi kila atakapopata wasaa.
Vile vile, mume ameshauriwa mara kwa mara apate muda wa kuongea, kufurahi na kufanya matembezi na mkewe. Tunajifunza katika hadithi nyingi kuwa Mtume (s.a.w.) alikuwa akifurahi na wakeze.
Kujizuia na kumchukia mkewe
Chuki ni kinyume cha upendo. Kumchukia mke ni ndoa kubwa katika nyumba, hivyo mwanamume anatakiwa ajitahidi kujiepusha na kumchukia mkewe, kwa kuyabeza maudhi madogo madogo yasiyo ya msingi kama Mtume (s.a.w.) anavyotushauri katika hadithi ifuatayo:
Abu Hurairah ameeleza kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu amesema: "Mwanamume aliyeamini na asimchukie mwanamke aliyeamini. Kama anachukia kipengele kimoja cha tabia yake, atafurahishwa na kipengele kingine kizuri katika tabia yake. (Muslim).
Hadithi hii inasisitiza kuvumiliana kwa kuyaangalia mazuri ya mtu na kuyafumbia macho mabaya yake. Kwani ni muhali mwanaadamu kukosa mabaya, angalau kidogo.
Kupigana na kuwa mkali kama pili pili
Mwanaume haruhusiwi kumpiga mkewe kwa makosa madogo madogo. Haruhusiwi kumpiga fimbo au kofi la usoni bali anaruhusiwa kumpiga kwa nguo au mti wa mswaki kiasi cha kumpa onyo. Kabla ya kufikia hatua hii ya kuwapeana maonyo Qur'an inatuelekeza tuwahame katika vitanda mpaka watakapo jirekebisha (4:34).
Mtume (s.a.w.) ametushauri katika hadithi mbali mbali kuwa, tuwe na subira na ustahamilivu juu ya wake zetu, kama tunavyojifunza katika hadithi ifuatayo:
Ilyas bin Abdullah ameeleza kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu amesema: "Msiwapige vijakazi vya Mwenyezi Mungu (s.w.) (wanawake). Kisha Umar alikuja kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu akasema: Wanawake wanawakalia (hawawajali) waume zao sasa. Kwa hivyo (Mtume) aliwaruhusu wawapige. (Kesho yake baada ya ruhusa hii) wanawake wengi wakawa wanaranda-randa katika mazingira ya nyumba ya Mtume wa Mwenyezi Mungu wakilalamika dhidi ya waume zao.
Mtume wa Mwenyezi Mungu akasema: "Wanawake wamerandaranda nyumbani kwa Muhammad wakilalamika dhidi ya waume zao. Wanaume hao sio wabora miongoni mwenu." (Abu Daud, Ibn Majah).
Hadithi hii inatuweka wazi kuwa, japo kupiga kunaruhusiwa, lakini kisiwe kipigo kikubwa cha kuumiza. Hata hicho kipigo hafifu si jambo linalopendeza mbele ya Mwenyezi Mungu (s.w.) na Mtume wake. Mtume (s.a.w.) ambaye ni kiigizo chetu, hatuoni popote alipothubutu kumnyoshea mkono, yeyote katika wake zake. Tunajifunza kuwa kutokana na ukorofi wa wakeze, aliwahi kuwahama kwa kipindi cha mwezi mmoja. Ili tuweze kuishi vizuri na wake zetu.
Kutunza siri za unyumba.
Ni jambo baya sana mbele ya Mwenyezi Mungu (s.w.) mtu kutoa siri za nyumbani kupeleka nje hasa zile zinazohusu unyumba. Utoaji wa siri za unyumba unaondoa uaminifu kati ya mke na mume, inaondoa upendo kati yao, na unatoa mwanya kwa maadui kuwaingilia na kuvunja nyumba yao.
Kuwa muadilifu
Mwanamume akiwa na mke zaidi ya mmoja, awe muadilifu na kuwagawia haki zao pasina upendeleo wowote. Ikitokea kuwa kuna kitu ambacho hakiwezekani kugawanyika itabidi wake zake wote waamue kwa pamoja kuwa nani kati yao apate kitu hicho kwa niaba ya wengine la sivyo itapigwa kura, na kitu hicho kitakuwa ni cha yule atakayeangukiwa na kura.
Mtume (s.a.w.) ambaye ni kiigizo chetu, alikuwa muadilifu mno na mwenye kugawa haki sawa kwa wake zake kama tunavyojifunza katika hadithi ifuatayo:
Aysha (r.a.) ameeleza kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu alikuwa akigawanya ngono kwa wake zake kwa usawa. Alikuwa akisema: "Ee Mwenyezi Mungu huu ndio mgawanyo wangu kulingana na uwezo wangu. Hivyo usinipatilize kwa kile ulicho na mamlaka nacho, ambacho mimi sina. (Tirmidh, Ahmed, Nisai).
Mtu kupendelea baadhi ya wakeze katika kuwapa haki zao, ni jambo baya mno, ambalo linaweza likawa ndio sababu ya mtu kuingia motoni kama tunavyojifunza katika hadithi ifuatayo:
Abu Hurairah ameeleza kuwa Mtume (s.a.w) amesema: Mtu mwenye wake wawili akawa anampendelea mmoja kati yao, atakuwa siku ya Kiyama na upande mmoja unaoning'inia chini. (Tirmidh, Abu Daud, Nisai).
Mwanaume akijitahidi kumpa mkewe haki zake na akawa muadilifu kwake, akajitahidi kuonesha mahaba kwake na akawa mvumilivu na mwenye subira juu ya udhaifu wake, kwa vyovyote vile atapendana na kushikamana vilivyo na mkewe endapo mkewe atakuwa ni Muumini na mcha-Mungu.
0 comments:
Post a Comment