ZAKA ZA FITRI NA SWALA YA EID
Allah
(Subhaanahu wa Taala) ametuwekea zaka za fitri kwa hikma ya kuwa ni kafara
pindi unapopatikana upungufu katika saumu ya Muislamu katika Mwezi wa
Ramadhani. Na hakika hakuna binadamu mkamilifu. Na Iddi imewekwa ili kuonyesha
kuwa Uislamu unazingatia maumbile ya binadamu, kwani binadamu huwa anapenda
kuwa na wakati wa kusherehekea, kwa ajili hiyo ndio ikawekwa Iddi mbili ili
ziwe sherehe zetu zimefungamana na ibada.
Kubainisha Maana ya Zaka za Fitri na
Hukumu yake.
Ni nini maana ya zaka za fitri?
Kabla
ya kueleza hilo, napenda kuwakumbusha waja wa Allah ya kuwa Mwezi Mtukufu wa
Ramadhani ni mgeni mtukufu aliyetujilia na amekurubia kuondoka. Inatakikana
tupatilize siku zillizobakia kwa wingi wa toba na amali njema huenda Mwenyezi
Mungu (Subhaanahu wa Taala) akaziunganisha amali zetu.
Enyi
waja wa Allah, Mwisho wa mwezi huu mtukufu kuna amali tukufu zenye kuzidisha
imani na kukamilisha ibada zetu, na amali hizo ni; zakatul fitri, takbira na
swala ya iddi. Na zakatul fitri ni sadaka ambayo inapasa kwa sababu ya kufungua
mwezi wa Ramadhani, na hakika imetambuliwa zaka za fitri kuwa ni swadaka ya
wajibu, kwa hivyo ndio tunaiita zaka za fitri sadakatul fitri. Sasa twende
katika kueleza hukumu ya zaka za fitri na dalili ya kuwekwa ibada hii.
Wanazuoni
wa fiq’hi wameafikiana ya kuwa zaka za fitri inampasa kila Muislamu mwenye
uwezo. Na dalili ni hadithi iliyopokewa na Ibnu ‘Umar asema katika mafhuum ya
maneno yake: Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) amefaradhishia watu
inapomalizika Ramadhani kutoa pishi ya tende au pishi ya ngano, na hilo ni kwa
kila Muislamu, awe muungwana au mtumwa, mume au mke”. Amepokea hadithi hii
Bukhari.
Hikma ya kuwekwa Zaka za Fitri :
Ni muhimu Muislamu kujua hikma ya zaka za fitri, hikma ya zaka
za fitri ni mambo mawili :-
1.
Hikma
ya kwanza ni kuwa inatwahirisha saumu ya mwenye kufunga. Kwani binadamu kwa
ubinadamu wake anaweza kufanya mambo ya kumpunguzia thawabu, basi hapo ndipo
inapokuja nafasi ya zaka za fitri. Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam)
ametuambia katika hadithi iliyopokewa na Ibnu ‘Abbas katika maana ya hadithi:
[Zaka za fitri ni twahara ya mwenye kufunga kutokana na upuuzi na maneno
machafu, na ni chakula kuwalisha maskini]. Imepokewa na Abu Daud.
2.
Hikma
ya pili ni kuwakunjua mafukara na maskini na kuingiza furaha nyoyoni mwao.
Masharti ya kutoa Zaka za Fitri
Zaka za Fitri ina masharti yake :
1.
Sharti
ya kwanza ni kuwa Muislamu. Kafiri si wajibu juu yake hata kama ana jamaa zake
Waislamu ambao ni wajibu kwake kuwalisha.
2.
Sharti
ya pili ni mtu kuwa huru sio mtumwa. Kwani Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi
wasallam) ametuambia: “ Watekelezeeni (zakatul fitri) kila huru na watumwa
mnaowalisha”.
3.
Sharti
ya tatu ni uwezo wa kimali nao ni kuwa na chakula cha siku moja na usiku wake.
4.
Sharti
ya nne ni kuingia wakati, nao ni kutwa jua la siku ya Iddi mwisho wa mwezi wa
Ramadhani. Na mwisho wa wakati wake ni baada ya kuswali iddi. Na mtu inafaa
aanze kujitolea yeye mwenyewe kwanza kisha amtolee anayepaswa kumlisha. Mtume
(Swalla Llahu ‘alayhi wasallam). ametuambia katika maana ya Hadithi : [Jianzie
na nafsi yako kisha unayemlisha].
Kiwango cha Zaka za Fitri na Vipimo vya Kisasa
Kiwango
cha zaka za fitri ni pishi moja ya ngano au wimbi au zabibu au chakula chochote
ambacho ni chenye kutumika sana mjini. Na pishi kwa kipimo cha kisasa ni kilo 2
na gramu 176.
Ibnu
‘Umar amepokea hadithi kutoka kwa Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam), ya
kuwa alifaradhisha zaka za fitri pishi ya mtama.
Na
wanazuoni wa fiq’hi wa madhehebu ya hanafi waliporuhusu kutoa thamani ya
kiwango cha chakula kinachopasa kutolewa ni kwa kuzingatia makusudio
yaliyokusudiwa katika kufaradhishwa zaka, nayo ni kuwakidhia maskini haja zao
katika siku hiyo ya iddi. Mu’adh amekubali kutoa thamani kwani ndio maslahi ya
mafukara. Na Ibnu Taimiyya amesema hakuna ubaya wa kutoa thamani.
Iddi katika Uislamu yakusanya Maana na Manufaa Makubwa
Kuna
akida ambayo ni safi na ni kupiga takbira na dua na kunyenyekea bila ya
kumshirikisha Mola, kama alivyosema Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala),
katika maana ya Aya:
(وَأَنَّ الْمَسَاجِدَ لِلَّهِ فَلَا تَدْعُوا مَعَ اللَّهِ أَحَدًا)
[الجن: 18]
{{Hakika Misikiti yote ni ya Mwenyezi Mungu, basi msiabudu yoyote
asiyekuwa Mwenyezi Mungu}}.
Na
iddi, kuna kubainisha hukmu za Mwenyezi Mungu kwa kudhihirisha Alama za
kiislamu. Na katika khutba kuna kufafanua hukumu za kiislamu kama vile
kusubiri, kusamehe na kuondosha chuki katika nyoyo, na kuonyesha uhusiano mwema
baina ya Waislamu. Kama alivyosema Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) katika
maana ya hadithi: [Watoshelezeni katika siku hii ya leo (yaani mafukara)].
Imepokewa na Daaraqutni kutoka kwa Ibnu Umar.
Baadhi ya Hukmu zinazopatikana katika Siku ya Iddi
kumtukuza
Mola wakati tukikamilisha hesabu. Allah (Subhaanahu wa Taala) Amesema:
فقال
تعالى: (وَلِتُكْمِلُوا الْعِدَّةَ وَلِتُكَبِّرُوا اللَّهَ عَلَى مَا
هَدَاكُمْ وَلَعَلَّكُمْ تَشْكُرُونَ) [البقرة: 185]
{{Ili
mkamilishe hisabu na mumtukuze Mwenyezi Mungu kwa kuwaongoza, na hakika
mutamshukuru}}.
Na kumeamrishwa hata wanawali na wenye hedhi watoke wapate
kushirikiana na Waumuni wenzao katika dua. Kama hadithi iliyopokewa na Ummu
‘Atia.
Ni
sunna kula tende au chochote katika iddil fitri kabla ya kwenda kuswali. Kama
alivyoeleza Anas sunna hii ya Mtume. Na Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala)
ametuambia, katika maana ya Aya:
قال الله عز وجل): لقد كَانَ لَكُمْ فِي رَسُولِ اللَّهِ
أُسْوَةٌ حَسَنَةٌ لِمَنْ كَانَ يَرْجُو اللَّهَ وَالْيَوْمَ الْآَخِرَ وَذَكَرَ
اللَّهَ كَثِيرًا ) [الأحزاب: 21]
{{Hakika mna kielezo chema kwa Mtume wa Allah kwa mwenye kumtarajia
Allah na siku ya mwisho na akamtaja Mwenyezi Mungu sana}}.
Mwisho
Tumeona
kama ilivyo tangulia ya kuwa idd ni kuchunga maumbile ya binadamu, na zaka ni
kuchunga maslahi ya mafukara na wasiojiweza na pia kurekebisha makosa madogo
madogo ambayo huenda binadamu asiye weza kuepukana nayo.
0 comments:
Post a Comment