KUJIANDAA NA MAISHA YA NDOA
UTANGULIZI
Shukurani zote ni kwa Allah
Subhaanahu Wata’ala aliyetakasika na aliyetukuka. Rehma na amani zimfikie
Mjumbe wake Swalla Allahu ‘Alayhi Wasallam aliyeletwa kwetu ili iwe ni rahma
kwa walimwengu wote.
Unapokaribia wakati wa kutaka kuoa/kuolewa, mume/mke mtarajiwa
hutingwa na masuala mengi vipi aanze kutafuta mchumba, sifa gani achague katika
kumpata mshirika wake wa maisha na vigezo gani atumie katika kufikia lengo
lake.
Masuala haya huwatinga watarajiwa na huku wakiwa na mitazamo
tofauti katika machaguo yao na mazoeya, desturi na tamaduni yakichangiya kwa
kiasi kikubwa katika kuathirika huko. Watarajiwa wengine
hawafahamu wanahitaji wake/waume wa aina gani, hivyo wanajikuta kama
wanaoingiya sokoni bila kujua wanataka kununua nini hasa.
Na jengine ni baadhi ya watarajiwa kujiingiza katika chuo cha
ndoa bila ya kupata taaluma yoyote inayohusiana na maisha hayo na hatimaye
kukosa uwezo wa kuziendesha ndoa zao.
Hata hivyo maandalizi haya huwa yanafanyika kwa kiasi kikubwa
katika idara nyenginezo na kwa ufanisi mkubwa ila tu katika suala la kimsingi
la dini, maandalizi haya huwa hayana nafasi wala kupewa kipaumbele na mara
nyingi huwa ni suala la mwisho linaloangaliwa kwa baadhi (likibahatika).
Kwa mtazamo uliokwisha zoeleka siku hizi, suala la ndoa limekuwa
ni suala zaidi la kijamii, desturi na kitamaduni na si suala la kidini kabisa
na athari zake ni kupewa kipaumbele masuala ya kijamii na kitamaduni na
hatimaye kuhatarisha msingi mkuu wa kidini ambao kila siku zikiendelea unazidi
kupoteza mwelekeo kwa kasi ya kutisha.
Katika uchaguzi wa mtarajiwa kuna mambo mawili yanaweza
kujitokeza nayo ni kuwa na ndoa iliyojaa matarajio ya watarajiwa (kama
yalikuwepo kabla) au kuwa na ndoa iliyokosa matarajio ya watarajiwa na hivyo
mwisho wake kuwa ni balaa badala ya raha na dhiki badala ya faraja. Anaweza mtu
kuoa/kuolewa na akafurahia uamuzi wake huo kwa jinsi ndoa ilivyotimiza matakwa
ya kuitwa ndoa na mwengine akajutia uamuzi wake kwa dhiki na maudhi mpaka
kufika kukhasimiana na kuachana.
Lengo na madhumuni ya mwongozo huu ni kujaribu kwa kiasi kidogo
tu kutoa ufafanuzi wa jinsi ya kujiandaa na suala zima la ndoa na ikiwa kama ni
mwongozo ambao utaangalia zaidi katika upande wa kidini wakati wa
maandalizi ya kuchumbia pamoja na kugusia sehemu nyengine muhimu.
Kuwepo na utulivu katika ndoa ni moja katika mambo muhimu ya
kuidumisha na kuiendeleza ndoa. Na mojawapo katika mambo yanayokosesha utulivu
katika ndoa zetu ni kutokana na chuo chenyewe cha ndoa kutopewa umuhimu wake
unaostahili na kutokuzingatia yale mambo ya kimsingi ambayo kwa ajili yake ndio
huamua kuchukua uamuzi wa kuoa/kuolewa.
Mwongozo huu umegawika sehemu kuu tatu, ya kwanza ikiwa ni
kuzungumzia umuhimu wa ndoa na kwa nini tunahitaji chuo hiki na sehemu ya pili
itagusia posa na jinsi ya kutambua vigezo vya atakayekuwa mshirika wa maisha na
sehemu ya tatu itagusia mume mtarajiwa na mke mtarajiwa na zaidi ni katika
kuzitambua haki na wajibu wa mume na mke ndani ya ndoa ya kiislamu pamoja na
nasaha kwa watarajiwa.
UMUHIMU WA NDOA
Moja katika alama zake Allah Subhaanahu Wata’ala ni kuisimamia
ndoa na kuiwekea taratibu zake maalum katika sheria tokea nguzo, adabu, fadhila
na hekima zake. Tukiangalia kitabu chake Allah Subhaanahu Wata’ala – Qur’aan
tunaona jinsi ilivyotudhihirishia mambo haya katika sehemu tofauti na kwa mfumo
maalum ambayo ni Qur’aan pekee ingeliweza kuifafanua katika sura hii.
Miongoni mwa mambo ambayo Qur’aan inazungumzia juu ya ndoa ni
1. Kuiamrisha
Kama anavyosema katika Suuratu Nnisaa/3
فَانكِحُواْ مَا طَابَ لَكُم مِّنَ النِّسَاء
Basi oeni mnao wapenda katika wanawake
Suuratu Nnuur/32
وَأَنكِحُوا الْأَيَامَى مِنكُمْ وَالصَّالِحِينَ مِنْ عِبَادِكُمْ وَإِمَائِكُمْ
Na waozeni wajane miongoni mwenu na wema katika watumwa wenu na
wajakazi wenu
2. Kuihamasisha
Kama anavyosema Allah Subhaanahu Wata’ala katika Arra’ad/38
وَلَقَدْ أَرْسَلْنَا رُسُلاً مِّن قَبْلِكَ وَجَعَلْنَا لَهُمْ أَزْوَاجًا وَذُرِّيَّةً
Na hakika Sisi tulikwisha watuma Mitume kabla yako, na tukajaalia
wawe na wake na dhuriya
3. Huleta
utajiri na wepesi katika maisha kama anavyosema katika Annuur/32
إِن يَكُونُوا فُقَرَاء يُغْنِهِمُ اللَّهُ مِن فَضْلِهِ وَاللَّهُ وَاسِعٌ عَلِيمٌ
Wakiwa mafakiri Allah atawatajirisha kwa fadhila yake. Na Allah ni
Mwenye wasaa Mwenye kujua
4. Ni njia ya kukiendeleza kizazi katika ardhi
Annahl/72
وَاللّهُ جَعَلَ لَكُم مِّنْ أَنفُسِكُمْ أَزْوَاجًا وَجَعَلَ لَكُم مِّنْ أَزْوَاجِكُم بَنِينَ وَحَفَدَةً وَرَزَقَكُم مِّنَ الطَّيِّبَاتِ أَفَبِالْبَاطِلِ يُؤْمِنُونَ وَبِنِعْمَتِ اللّهِ هُمْ يَكْفُرُونَ
Na Allah amekuumbieni wake katika jinsi yenu, na akakujaalieni
kutoka kwa wake zenu wana na wajukuu, na akakuruzukuni vitu vizuri vizuri.Basi
je, wanaamini upotovu na wanazikataa neema za Allah?
5. Ni njia ya kupatikana utulivu, stara,
mapenzi na kuoneana huruma.
Arruum/21
وَمِنْ آيَاتِهِ أَنْ خَلَقَ لَكُم مِّنْ أَنفُسِكُمْ أَزْوَاجًا لِّتَسْكُنُوا إِلَيْهَا وَجَعَلَ بَيْنَكُم مَّوَدَّةً وَرَحْمَةً إِنَّ فِي ذَلِكَ لَآيَاتٍ لِّقَوْمٍ يَتَفَكَّرُونَ
Na katika Ishara zake ni kuwa amekuumbieni wake zenu kutokana na
nafsi zenu ili mpate utulivu kwao. Naye amejaalia mapenzi na huruma baina yenu.
Hakika katika haya bila ya shaka zipo Ishara kwa watu wanaofikiri.
6. Huunganisha koo kufikia kuweza kurithiana kati ya mume na mke.
Annisaa/12
وَلَكُمْ نِصْفُ مَا تَرَكَ أَزْوَاجُكُمْ إِن لَّمْ يَكُن لَّهُنَّ وَلَدٌ فَإِن كَانَ لَهُنَّ وَلَدٌ فَلَكُمُ الرُّبُعُ مِمَّا تَرَكْنَ مِن بَعْدِ وَصِيَّةٍ يُوصِينَ بِهَا أَوْ دَيْنٍ
Na fungu lenu ni nusu walicho acha wake zenu ikiwa hawana mtoto.
Wakiwa na mtoto basi fungu lenu ni robo ya walicho acha, baada ya wasia waliyo
usia au kulipa deni. Na wake zenu watapata robo mlicho kiacha, ikiwa hamna
mtoto. Mkiwa mna mtoto basi sehemu yao ni thumni ya mlicho kiacha, baada ya
wasia mlio usia au kulipa deni
Ndoa, katika mtazamo wa kisheria, ni msingi wa kwanza katika
kujenga jamii ya kiislamu iliyo safi na tohara ikipelekea kuwepo utulivu katika
jamii hii na kuhakikishiwa malipo mema huko akhera kwani ni mojawapo katika
mambo ambayo yataweza kutuingiza katika pepo ikiwa tutakamilisha na kutekeleza
vizuri misingi na taratibu za ndoa.
Miongoni mwa Hadithi za Mtume Swalla Allahu ‘Alayhi Wasallam
zinazozungumzia juu ya ndoa ni
1. Kuiamrisha
: يا معشر الشباب من استطاع منكم الباءة فليتزوج؛ فإنه أغض للبصر وأحصن للفرج، ومن لم يستطع فعليه بالصوم، فإنه له وجاء. متفق عليه.
Enyi vijana mwenye kuweza miongoni mwenu kuoa na aoe kwani (ndoa
huleta) kuinamisha macho na kinga kwa utupu na asieweza basi na afunge kwani
hiyo ndiyo kinga. Bukhaari na Muslim
2. Kuilinda
: ثلاثة حق على الله عونهم: المجاهد في سبيل الله، والمكاتب الذي يريد الأداء، والناكح الذي يريد العفاف
رواه الترمذي وغيره وحسنه الألباني
Watu watatu ni haki yake Allah kuwasaidia; mwenye kupigana
jihadi kwa ajili ya Allah, mwenye kuandikiana na Mtumwa (Kwa ajili ya kuachiwa
huru) huku akiwa na nia ya kulitekeleza hilo, na mwenye kutaka kuoa akitaka
kupata sitara na kujizuia na maovu.”
Attirmdhiy na wengineo na Sh.
Albaani anasema ni Hadithi Hasan
3. Hukamilisha nusu
ya dini
: إذا تزوج العبد فقد استكمل نصف الدين فليتق الله فيما بقي. صححه الشيخ الألباني في السلسلة الصحيحة
"Mwenye kufunga ndoa (atakuwa) amekamilisha nusu ya Imani
(dini yake) na amuogope Allah katika nusu itakayobakia" Ameisahihisha Sh. Albaani katika Silsila Sahiha
4. Kuiraghibisha
"إذا أتاكم من ترضون خلقه ودينه فزوجوه إن لا تفعلوا تكن فتنة في الأرض و فساد عريض
صحيح الجامع
Atakapokujieni
mtakaemridhia kwa tabia zake na dini yake basi muozesheni na kama hamkufanya
itakuwa fitna katika ardhi na ufisadi mkubwa. Sahihul Jaami’i
5. Ndiyo starehe ya dunia
"الدُّنْيَا مَتَاعٌ وَخَيْرُ مَتَاعِ الدُّنْيَا الْمَرْأَةُ الصَّالِحَةُ" مسلم
Dunia ni starehe.
Na starehe iliyo bora kwa dunia ni mwanamke aliye mwema. Muslim
Pia ndoa ni
muhimu kwa sababu
· Huitekeleza Sunna
ya Mtume Swalla Allahu ‘Alayhi Wasallam.
· Hupata jamii
iliyojengeka katika misingi sahihi.
· Huiepusha jamii
na tabiya chafu ambazo wasiooa hupendelea kuzitekeleza.
· Huiepusha jamii
na maradhi mengi.
· Kuwapa wanandoa
hisia ya kwamba wao pia wanapendwa kama wanavyojipenda wao wenyewe.
· Hupatikana
utajiri.
· Huifundisha jamii
maana halisi ya kubeba majukumu.
YA KUZINGATIYA KABLA YA
KUOA/KUOLEWA
· Ndoa ni moja
katika alama na miujiza ya Allah Subhaanahu Wata’ala.
· Ndoa ni mojawapo
ya rizki ambazo Allah Subhaanahu Wata’ala hugawa kwa waja wake.
· Ndoa ina haki,
majukumu na uwajibikaji.
· Upungufu katika
kutekeleza majukumu na kuwajibika ni mojawapo katika sifa za binadamu
(aliyekamilika ni Allah Subhaanahu Wata’ala pekee).
· Ndoa ina mitihani
na majaribu.
KWA NINI KUOA/KUOLEWA?
Jibu la suala hili ni muhimu. Ndiyo kitu cha kwanza kukiangalia
kwa ukweli na moyo mkunjufu kwa kila anaejiandaa na ndoa. Kitu gani
kinachotupelekeya kuoa/kuolewa? Hapa kuna mambo mengi kama:
· Kupata nafasi ya
hadhi na heshima katika jamii
· Kupata watoto
· Kutafuta sitara
· Kujenga familiya
bora
· Kuwaridhiya
wazazi wawili
· Kukidhi
hamu/shahawa za kijinsia
· Kufuata
marafiki/mashoga na kadhalika
· Kupata mtu wa
kupika na kuosha nguo na kadhalika
· Kupata mali na
utajiri
· Kuepuka lawama na
maudhi
Mifano hii inatupa picha kwamba kwa wanaoingia kwenye chuo cha
ndoa huwa na malengo na sababu tofauti kulingana na hali na mazingira yao.
Tuangalie hadithi ya Mtume Swalla Allahu ‘Alayhi Wasallam ambayo
pia inatufahamisha mambo ya kimsingi ambayo kwayo mwanamke huolewa.
Hakika Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam amesema:
تنكح المرأة لأربع: لمالها ولحسبها ولجمالها ولدينها، فاظفر بذات الدين تربت يداك.
البخاري ومسلم
Mwanamke huolewa kwa mambo mane: Kwa (ajili ya) mali yake, kwa
nasaba yake, kwa uzuri wake na kwa dini yake, basi mtafuteni mwenye dini
(kwani) mikono yako itatakatika na michanga. Bukhaari na Muslim
Na pia Amesema:
: إذا تزوج العبد فقد استكمل نصف الدين فليتق الله فيما بقي. صححه الشيخ الألباني في السلسلة الصحيحة
"Mwenye kufunga ndoa (atakuwa) amekamilisha nusu ya Imani (dini
yake) na amuogope Allah katika nusu itakayobakia” Ameisahihisha Sh. Albaani katika Silsila Sahiha.
Hapa ndipo umuhimu wa kujua lengo kabla ya tendo linapokuja. Kwani
ndoa ni moja katika miundo mbinu ya jamii na hivyo ni vyema lengo likafahamika
mapema na liwe katika sura na mtazamo sahihi kama tunavyosisitiziwa na Mtume
wetu Swalla Allahu ‘Alayhi Wasallam.
HEKIMA YA KUWEPO NDOA
1. Kuitikiwa wito wa Allah Subhaanahu Wata’ala na Mtume wake Swalla
Allahu ‘Alayhi Wasallam
2. Kupata ujira na thawabu
KWA NINI WENGINE HAWAFIKIRII NDOA?
Inawezekana kwa sababu tofauti kama
1 Sababu za kisaikolojiya
· Kuwa na khofu na wasiwasi
· Kuwa na udhaifu wa kudhani watashindwa kutimiza majukumu
2 Sababu za Kijamiii
· Ughali wa mahari
· Kusubiri mpaka mmojawapo awe tayari kwa ndoa
· Kusubiri kupata ajira, kazi au kibarua
· Kutofautiana kati ya wazazi na mtoto katika chaguo.
3 Sababu za kijinsia
· Kuweza kujitosheleza kijinsia kwa njia
za haramu(zinaa)
4 Sababu za kielimu
· Kuendelea na
masomo
Licha ya kuwepo sababu zote hizi turudi katika dini yetu na
tuangalie kitu gani tunausiwa na Mtume wetu Swalla Allahu ‘Alayhi Wasallam
katika suala zima la ndoa kwa mwenye uwezo wa kuhimili.
KWA NINI WENGINE HUCHUKIYA NDOA?
Ni kwa sababu tofauti kama
· Kulazimishwa
kuolewa na mume asiyemtaka
· Kulazimishwa kuoa
mke asiyemtaka
· Kuchelewa kuoa
kwa kukosa uwezo
· Kutegemeya sifa
za ujumla za familiya bila ya kufuatilia kwa undani
· Kumuandaa na
kumwambia mtoto tokea utotoni kwake kwamba atamuoa/ataolewa na fulani
· Kutosimama kwa
posa kwamba kila zikija huwa zinarudi.
· Kuzuiliwa mwanamke
kuolewa kwa khofu na wasiwasi usiokuwa na msingi wa kidin
0 comments:
Post a Comment