Aina Za Ndoa Na Hukumu Zake
Katika makala hii fupi inshaAllaah tutajaribu kuzitambulisha aina za ndoa na kuweza kuzijua hukumu zake kisheria pamoja na maelezo kwa ufupi.
Ndoa ni miongoni mwa alama na miujiza yake Allaah (Subhaanahu Wata’ala) na ina dalili ya kuthibitika kwake katika Qur’aan na katika Sunnah.
Katika Qur’aan
Suuratu Nnisaa/3
وَإِنْ خِفْتُمْ أَلاَّ تُقْسِطُواْ فِي الْيَتَامَى فَانكِحُواْ مَا طَابَ لَكُم مِّنَ النِّسَاء مَثْنَى وَثُلاَثَ وَرُبَاعَ فَإِنْ خِفْتُمْ أَلاَّ تَعْدِلُواْ فَوَاحِدَةً أَوْ مَا مَلَكَتْ أَيْمَانُكُم
“Na ikiwa mnaogopa kuwa hamtowafanyia mayatima uadilifu, basi oeni mnaowapenda katika wanawake, wawili au watatu au wanne. Na mkiogopa kuwa hamwezi kufanya uadilifu, basi mmoja tu, au wale ambao mikono yenu ya kulia imewamiliki.”
Suuratu Nnuur/32
وَأَنكِحُوا الْأَيَامَى مِنكُمْ وَالصَّالِحِينَ مِنْ عِبَادِكُمْ وَإِمَائِكُم
“Na waozeni wajane miongoni mwenu na wema katika watumwa wenu na wajakazi wenu.”
Katika Sunnah
يامعشر الشباب ، من استطاع منكم الباءة فليتزوج فإنه أغض للبصر وأحصن للفرج ، ومن لم يستطع فعليه بالصوم فإنه له وجاء
أخرجه البخاري
“Enyi vijana! Mwenye uwezo wa kuisimamia ndoa na aoe kwani huko ni kuweza kuinamisha macho na kuweza kuzikinga tupu na kama hamna uwezo basi ni juu yenu kufunga kwani huko ndiko kwenye kinga.” Al-Bukhaariy
Na pia:
النكاح من سنتي ، فمن لم يعمل بسنتي فليس مني
Ndoa ni miongoni mwa Sunnah zangu na mwenye kutenda kinyume na Sunnah zangu hatokuwa pamoja na mimi. Ibn Maajah
Ili ndoa ikamilike hupaswa kutimiza nguzo, masharti pamoja na adabu zake vinginevyo inaweza kuwa miongoni mwa ndoa zenye utata katika uhalali wake.
Ndoa, kwa mujibu wa Rai za Jamhuur Ulamaa (isipokuwa Abu Haniyfah), zimegawika kwenye sehemu kuu tatu zifuatazo:
1 Ndoa sahihi iliyokamilika
Iliyotimiza nguzo na masharti ya kusihi kwake na kuweza kutekelezwa.
2 Ndoa Sahihi isiyokamilika
Iliyotimiza nguzo na masharti ya kusihi kwake lakini imeshindwa kutekelezwa.
3 Ndoa batili au fasidi
Iliyokosekana moja ya nguzo au masharti ya kusihi kwake.
Yanayopaswa kuwepo wakati wa kufungwa ndoa (Aqdi)
Ni yafuatayo
1 Kuwepo mke na mume (ambao wataweza kuisimamia ndoa na kutokuwepo vizuizi vya kuwazuia kuoana)-miongoni mwa masharti ya ndoa.
2 Ijaabu (tamko la kuoa au kuozesha) na Qabuul (tamko la kukubali) – miongoni mwa nguzo za ndoa
3 Awepo walii -miongoni mwa masharti ya ndoa
4 Wawepo Mashahidi – miongoni mwa masharti ya ndoa
Yanayopaswa kuzingatiwa
Ni yafuatayo
- Asiwe mmoja wa wanandoa ana vizuizi vya kuwafanya wasioane ikiwa ni vya muda au vya kudumu.
- Mkataba wa ndoa uwe wa kudumu usiwekewe muda maalum.
- Ridhaa, chaguo na uamuzi uwe ni wa wanandoa kusiwepo kulazimishana.
- Wasiwe wanandoa katika hali ya kuhirimia kwa ajili ya Hajj au ’Umrah.
- Yawepo mahari.
- Wajulikane wanaooa au kuolewa.
- Kusiwepo mbinu za kutoitangaza ndoa na kuificha.
Ndoa batili au fasidi
1 | NDOA FASIDI/ BATILI | Iliyofisidika kwa kukosekana moja katika nguzo, masharti ya msingi ya kufungika ndoa. | Ndoa hutakiwa ikamilike mambo yake yote zikiwemo nguzo masharti ya kusihi kwake ili iweze kuwa na uhalali kisheria. | Haijuzu |
2 | NDOA WAKATI WA IHRAAMU | Kuoa/kuolewa wakati mmeshahirimia ima kwa ibadah ya Hajj au ‘Umrah. | Kuwepo katika hali ya Ihraamu ni moja katika mambo yanayomzuia mke/mume kufanya tendo la ndoa na kuoa au kuwakilishwa ndoa pia ni mambo yasiyofanywa kwa aliye kwenye Ihraamu. | Haijuzu |
3 | NDOA BILA YA WALII | Kufungwa ndoa kwa kuwepo mke na mume pamoja na mashahidi lakini Walii amekosekana. | Ndoa haikamiliki bila ya kuwepo kwa Walii na ni mojawapo ya nguzo za ndoa. Walii ni mwenye haki ya kumuozesha na kusimamia ndoa kwa niaba ya binti. | Haijuzu kwa mujibu wa Jamhuur Ulamaa na inajuzu kwa mwanamke aliye baleghe kujiozesha kwa mujibu wa rai ya Abu Haniyfah. |
4 | NDOA YA “WALII” ASIYEKUWA NA SIFA | Kufungwa ndoa kwa kutimizwa masharti yote isipokuwa walii ni mama wa binti kwa kukosekana baba na mfano wake. | Moja katika masharti ya kusihi ndoa ni kuwepo walii mwanamme. Kisheria walii ni mwanamme na mwanamke si miongoni mwa walii wa binti. | Haijuzu |
5 | NDOA BILA YA KUWEPO MASHAHIDI | Kufungwa ndoa wakiwepo mke na mume na walii bila ya kuwepo shahidi kama ilivyo ndoa ya Mut’ah au ndoa ya siri | Ni moja katika masharti ya kusihi ndoa kwamba lazima ishuhudishwe na mashahidi ili kuondosha dhana ya kuwepo ndoa za siri na kuondosha tuhuma na dhana. | Haijuzu |
Ndoa zenye utata katika kujuzu kwake
NDOA | MAELEZO | SABABU | HUKUMU | |
1 | NDOA YA MUT’AH (MUDA MAALUM) | Hufungwa kwa muda maalum japo masaa mawili, bila mashahidi wala walii, ambapo wanandoa kuwa na haki kama wameoana. | Imewekewa muda maalum na hakuna kurithiana wala kutalikiana. | Haijuzu |
2 | NDOA YA MHALILI (ALIYEACHIKA TALAKA TATU) | Kuolewa mke aliyeachika talaka tatu si kwa lengo la ndoa bali kwa lengo la kuipinda sheria ili ahalalishiwe mume wa mwanzo. | Mume anataka kurudiana na mkewe ambaye kamuacha talaka tatu na hivyo kumtafuta mume mwengine amuoe mkewe kwa makubaliano lakini pasipatikane tendo la ndoa kisha amuache.
Kisheria atatakiwa aolewe na mume mwengine ndoa halisi na papatikane tendo la ndoa.
| Haijuzu |
3 | NDOA ZAIDI YA WAKE WANE | Mume kuoa wake zaidi ya wane kwa wakati mmoja waliokubalika kisheria. | Ruhusa na mipaka tuliyowekewa na sheria ni kuwa na wake wane tu kwa wakati mmoja. (Na hata kama mke ameachika talaka rejea na yupo katika eda basi uharamu upo pale pale). | Haijuzu |
4 | KUOLEWA NA MUME ZAIDI YA MMOJA WAKATI MMOJA | Mke kuolewa na mume zaidi ya mmoja kwa wakati mmoja yaani kuwa na waume wawili na kuendelea. | Sheria inakataza mke kuolewa na waume wengi kwa wakati mmoja kwani ni kinyume na fitrah- maumbile ya asli (Uislamu). | Haijuzu |
5 | NDOA KWENYE EDA | Kumuoa au hata kumposa mke aliyeachika na bado yupo katika eda na hakuwa mke wake kabla. | Kuwepo kwenye eda ya aina yoyote kwa mke ni kizuizi kinachomfunga kutoweza kuolewa mpaka imalizike isipokuwa kwa mtalaka wake tu kama mke aliyeachika talaka rejea. | Haijuzu |
6 | NDOA KWENYE UJA UZITO KWA MWANAMKE AMBAYE HAJAPATA KUOLEWA KABLA | Kwa mwanamke ambaye hajaolewa akazini na kupatikana ujauzito na kutaka kuolewa katika hali hii. Ndoa hizi hufanyika pale mambo yameshaharibika na kutaka kusitiriana | Ujauzito utakuwa na hukumu sawa kama mwanamke aliye katika eda (Ahmad na Abu Haniyfah). Uja uzito hautokuwa na hukumu sawa kama mwanamke aliye katika eda (Maalik na ash-Shafi’iy). | Haijuzu kwa rai ya Ahmad na Abu Haniyfah
Inajuzu kwa rai ya Maalik na ash-Shafi’iy ila tu hatopaswa kustarehe naye mpaka ajifungue.
|
7 | NDOA KWENYE UJA UZITO KWA ALIYEACHIKA | Mke aliyeachika na ni mja mzito na kutaka kuolewa na mume mwengine asiyekuwa mtaliki wake. | Mke aliyeachika katika uja uzito yupo katika Eda na humalizika atakapojifungua na kumaliza muda wake wa Nifasi. Kisheria Eda inamfunga mke kuolewa mpaka imalizike. | Haijuzu |
8 | NDOA KWA ASIYEKUWA MUISLAMU WALA HAKUTEREMSHIWA KITABU | Kuoa washirikina na makafiri ambao si miongoni mwa walioteremshiwa vitabu kama mayahudi na manasara. | Moja katika masharti ya kusihi ndoa ni Uislamu. Hivyo kuoa asiyekuwa Muislamu huifanya ndoa kuwa fasidi. | Haijuzu |
9 | NDOA KWA ASIYE MUISLAMU LAKINI NI MIONGONI MWA WALIOTEREMSHIWA KITABU | Walioteremshiwa vitabu miongoni mwa mayahudi na manasara na wanaowafuata katika mila zao. | Uislamu ni moja ya masharti ya kusihi ndoa ila kwa mujibu wa aya za Qur’aan wameruhusika kuolewa. | Inajuzu ingawa ni Makruuh – haipendezi |
10 | KUOLEWA MUISLAMU NA ASIYEKUWA MUISLAMU | Mwanamke wa Kiislamu kuolewa na kafiri, mwenye kumshirikisha Allaah pamoja na mayahudi na manasara. | Ndoa hulazimisha utiifu wa mke kwa mumewe na hivyo kuwepo khofu ya kuweza kuathirika na kubadilisha dini na watoto kufuata dini ya baba. | Haijuzu |
11 | KUOA/KUOLEWA NA ALIYERTADI | Mwanamme au mwanamke aliyekuwa Muislamu kisha akaamua kurtadi – kutoka katika dini. | Kwa kukosekana sharti la msingi la Uislamu na hata kama atakuwa amekwenda katika dini ya walioteremshiwa vitabu. | Haijuzu |
12 | KUMUOA BINTI ULIYEZAA NJE YA NDOA | Mwanamme kuoa binti aliyezaa baada kutembea (kuzini) na mama yake nje ya ndoa. | Huyu ni mtoto wake kwani ni mbegu zake ila tu atakosa baadhi ya haki za kimsingi kwa kuzaliwa nje ya ndoa. | Haijuzu |
13 | KUOA BINTI WA KAMBO AMBAYE MLIWAHI KUWA NA MAHUSIANO HARAMU NA MAMA YAKE | Kuoa binti wa kambo ambaye mliwahi kuwa na uhusiano haramu (zinaa) na mama yake kabla. Si binti aliyezaa nje ya ndoa bali ni binti wa mama. | Kutokana na kupatikana tendo la haramu la zinaa Maulamaa wametofautiana katika tendo hili (zinaa) je llitaweza kuharamisha halali (ndoa)? Na kuna Qaaidah-“Haramu haiwezi kuifanya halali nyengine kuwa haramu”. Kuna Qaaidah nyengine “tendo la haramu huharamisha halali”. | Inajuzu kwa rai ya ash-Shaafi’iy na Maalik kwa sababu ya kutokuwepo dalili bayana kuharamisha. Haijuzu kwa rai ya Abu Haniyfah na Ahmad bin Hanbal kwa sababu ya kuwepo tendo la haramu zinaa. |
14 | KUOA BINTI WA KAMBO AMBAYE MLIWAHI KUWA NA MAHUSIANO HALALI NA MAMA YAKE | Kuoa binti wa kambo ambaye kuliwahi kuwepo mahusiano ya halali (ndoa) na mama yake mzazi na binti huyu si miongoni mwa watoto wa mume. | na Qaaidah – msingi wa kisheria yakipatikana maingiliano kwa mama huharamisha (kuolewa) binti yake. | Haijuzu |
15 | KUOA MAMA AMBAYE ULIWAHI KUOA BINTI YAKE | Kumuoa mama ambaye kabla mliwahi kuwa na uhusiano wa ndoa na binti yake. | Haijuzu | |
16 | NDOA KWA WALIONYONYA ZIWA MOJA | Ikiwa watoto wa kike na wa kiume wametokezea kunyonya ziwa moja kwa mama mmoja na wakataka kuoana. | Moja katika mambo yanayoharamisha ndoa ni kuoa /kuolewa na mliyenyonya ziwa moja kwani kitendo hiki tayari kisheria kimeshaunda udugu baina yao. | Haijuzu |
17 | NDOA YA KUBADILISHANA (SHIGHAAR) | Mwanamme kumuozesha binti/dada yake kwa mwanamme mwengine ambaye naye atamuozesha binti/dada yake kwa mwanamme wa mwanzo kwa mabadilishano. | Ndoa hizi hufanyika pasi na kutajwa mahari kwani mahari ya kila mmoja ni kumkubalia mwengine kuoa kwake “nipe nikupe” na pasi na kupatikana ridhaa ya upande mwengine. | Rai yenye nguvu haijuzu kwa kufanyika kinyume na misingi ya ndoa ya Kiislamu. |
18 | NDOA YA BOMANI | Ndoa zinazofungishwa na wakuu wa wilaya au kwenye ofisi za wasajili wa ndoa serikalini. | Hufanyika bila ya kutekelezwa masharti ya kimsingi katika sheria za ndoa za Kiislamu kwani si lazima kuwepo mashahidi au kuwa wanandoa ni wa dini moja. | Haijuzu.
Ikiwa taratibu za nchi zinahitaji kufungwa ndoa hii itawajibika kwanza kufungwa ndoa ya Kiislamu.
|
19 | NDOA YA MISYAAR | Mwanamke hukubali kuolewa huku akisamehe baadhi ya haki zake za kimsingi katika ndoa kama mahari, huduma na makaazi au hata katika kugawana siku (kwa wake wenza). | Ndoa hizi hufanyika sana katika Bara Arabu hasa kutokana na ughali wa mahari na hivyo mke katika kutafuta stara huzisamehe baadhi ya haki zake.
Na pia kama wenye kuoa Afrika huku wakiwa na mke mwengine na hivyo mke wa Afrika kusamehe baadhi ya haki zake kama za kugawana siku na nyenginezo kwa kuwa anapata huduma nyengine kama pesa na kadhalika.
| Itajuzu ikiwa imetimiza masharti ya kimsingi – Haitojuzu ikiwa haitotimiza masharti ya kimsingi kama kufanyika ndoa ya Misyaar bila ya Walii. |
20 | NDOA YA MISFAAR | Hufungwa kwa muda maalum kama wakati wa mapumziko au kwa wafanyakazi, wanafunzi ambao wako mbali na miji au nchi zao humalizika baada ya kurudi sehemu zao walikotoka | Kimsingi ndoa yoyote itakayowekewa mkataba/muda maalum kumalizika kwake haikubaliki kisheria kama ilivyo Mut’ah. Mfano wanandoa wamekubaliana kuoana wakiwa Uingereza tu lakini wakirudi walipotoka ndoa imemalizika hata bila ya talaka. | Haijuzu kwa rai ya Jamhuur
Licha ya kutimiza masharti yote ya kimsingi ila kwa kuwepo muwafaka wa kumalizika kwake ambao ni kinyume na taratibu za ndoa ya Kiislamu.
Itajuzu kwa rai ya Abu Haniyfah ikiwa sharti la kumalizika halitozingatiwa kwani ni sharti batili.
|
21 | KUOA MWANAMKE ALIYEPOSWA KABLA | Kuvunja uchumba uliopo na kuposa kisha kumuoa binti ambaye tayari ameshachumbiwa. | Kwenda kuposa mwanamke aliyeposwa ni haramu kisheria. Kwa mujibu wa Hadithi za Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam. Ikiwa atakayeposa anajua taarifa za kuposwa kwa binti kabla basi
mtendaji ni mwenye madhambi na dhimma kwa kukiuka makatazo.
Kama hakujua na kufahamu baadae basi uharamu upo pale pale
| Ndoa itajuzu kwa mujibu wa rai ya Jamhuur Ulamaa kwa sababu kilicho haramu kilitokea kabla ya kufungwa na si katika ndoa kwani khutba si miongoni mwa mwa masharti ya kusihi ndoa.
Haijuzu kwa mujibu wa Maalik na kama ndoa itafanyika itabidi ibatilishwe
|
22 | NDOA YA KUJIFICHA “SIRI” | Kuoana kwa kukamilisha nguzo na masharti yote ya ndoa ila tu wanandoa na mashahidi kutakiwa kutoitangaza na kuidhihirsha. | Ikiwa ndoa hii itakamilika katika idara zote ila kilichokosekana ni mashahidi tu kuitangaza ndoa. Kama kuoa mke wa zaidi ya mmoja bila ya kumtaarifu mke/wake/watu wengine. | Inajuzu kwa sababu ndoa imekamilika kuwepo mashahidi kumeifanya si siri tena, imeshatangazwa. Ila ni jambo lisilopendeza kisheria (makruuh) |
24 | KUOA KWA NIA YA KUACHA | Mume kuoa na katika mkataba wa ndoa akashurutisha kwamba atamuacha mke katika muda fulani au bila ya kushurutisha lakini tayari ameshaweka nia katika nafsi yake ya kuacha. | Kimsingi ndoa yoyote itakayowekewa mkataba/muda maalum kumalizika kwake haikubaliki kisheria ikiwa imeshurutishwa au kuwekwa nia kwani inakuwa ndoa ya muda maalum. Na kuwepo ndani yake hadaa na udanganyifu. | Haijuzu kwa rai ya Jamhuur kwa sababu ya kuwekewa muda wa kumalizika na udanganyifu.
Itaweza kujuzu kwa rai ya Abu Haniyfah ikiwa shurti litabatilishwa na kutenguliwa
|
Ni muhimu kwa kila Muislamu kuzifahamu vyema aina hizi na kuhakikisha ndoa yake imefungwa katika misingi na taratibu zilizo sahihi. Na kama ni miongoni mwa watakaosimamia au kuwakilisha katika ndoa wazingatie maelezo haya ili waweze kuwa na uelevu katika mwenendo mzima wa ndoa kuepuka matatizo na kuepukana na ndoa zenye utata.
Pia kuwepo tayari kuusimamia ukweli na haki pale ambapo ndoa iliyofungwa ilifungwa katika misingi isiyokuwa sahihi au baadhi ya taratibu zake kukiukwa.
Ikiwa ndoa ni moja katika alama zake Allah Subhaanahu Wata’ala na miujiza yake hatuna budi Waislamu kuhakikisha kuzithibitisha alama hizi kwa kuifunga katika misingi na taratibu sahihi za kisheria.
Na Allah Ndiye Ajuaye zaidi
0 comments:
Post a Comment