NGUZO ZA UDHU
Kabla hatujaanza kuzielezea na kuzibainisha nguzo za
udhu moja baada ya nyingine kama zilivyotajwa ndani ya Qur-ani Tukufu, ni vema
kujiuliza nguzo ni nini ?
Makusudio ya neno Nguzo hapa ni yale mambo ambayo
dhati na hakika ya udhu unayategemea kiasi ambacho likikosekana au kupungua
moja miongoni mwao, udhu huwa ni batili kisheria.
Hiyo ndiyo maana na muradi wa nguzo na zifuatazo sasa
ndizo hizo nguzo za udhu kwa utaratibu; ambazo ni sita :
1.NIA 2.KUOSHA USO MZIMA
Hii ndio nguzo ya kwanza ya udhu. Neno “nia” lina
maana mbili; maana ya kilugha na maana ya kisheria. Nia katika lugha ya kawaida
ni MAKUSUDIO na katika lugha ya kisheria ni MAKUSUDIO YA KITU/JAMBO HALI YA KUAMBATANISHA KITU/JAMBO
HILO NA KITENDO CHAKE.
Na nia hukaa moyoni mwa mtu. Dalili/ushahidi wa
kufaradhiwa nia ni kauli ya Bwana Mtume –Rehema na Amani zimshukie –
“Hakika (kusihi kwa) amali kumefungamana na nia na
kila mtu (atalipwa) kwa mujibu wa nia (yake) ……”Al-Bukhariy na Muslim.
Kwa kuwa udhu
ni ibada na kwa kuwa nia ndiyo hupambanua baina ya ibada na ada; ikaonyesha
kuwa hili sasa ni tendo la ibada kama josho la wajibu na hili ni tendo la ada
kama josho la unadhifu.
Basi kwa
mantiki hii ikawa ni lazima udhu uambatane na nia. Namna ya nia ni mtu kusema
moyoni mwake :
“Nawaytu Fardhal-udhui” au
“Nawaytu Raf-al Hadath” au
“Nawaytu istibihatas-swalaat”
“Nawaytu Raf-al Hadath” au
“Nawaytu istibihatas-swalaat”
Nia Huletwa wapi na mawakati gani ?
Nia huletwa wakati wa kuosha fungu/sehemu ya mwanzo ya
uso, kwa kuwa hapo ndio mwanzo wa udhu yaani udhu unaanzia hapo na yaletwayo
kabla ya hapo huhesabika kama maandalizi ya kuingia ndani ya udhu.
2.KUOSHA USO MZIMA/WOTE
kwa kufuata kauli
ya Mwenyezi Mungu Mtukufu :
“BASI OSHENI
NYUSO ZENU …”[5:6]
Kuosha uso
mzima ndio nguzo ya pili ya udhu.
Uso huoshwa
mara moja tu kwa kuitegemea kauli ya Mtume :
“Udhu
ni mara moja moja”.
Ama kule
kuosha mara ya pili na ya tatu ni suna.
Imethibiti
riwaya kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu –Rehema na Amani zimshukie – alitawadha
mara moja moja na akasema :
“Huu
ndio udhu ambao Allah haikubali swala ila kwao” Na akatawadha (tena) mara mbili mbili na akasema :
“Huu ndio wa wa mtu ambaye Allah atampa ujira mara mbili” Na akatawadha (tena) mara tatu tatu na
akasema :
“Huu
ndio udhu wangu na udhu wa mitume kabla yangu, basi atakayezidisha (zaidi ya)
hivi au kupunguza, (huyo atakuwa) amechupa mipaka na kufanya dhuluma”
Uso ni upi ?
Kisheria uso huanzia maoteo/mameleo ya nywele za kichwa mpaka chini ya kidevu,
huo ni urefu, na upana wake ni tokea ndewe moja ya sikio hadi nyingine.
Eneo lote
lililo katika mipaka hiyo, ndio huitwa uso katika sheria.
Na ni wajibu
kuosha kila kilichoota ndani ya mipaka hiyo kama nyusi, kope, sharubu na ndevu.
Ndevu huoshwa nje na ndani zikiwa chache.
Ama zikiwa ni
nyingi zilizoshindamana kiasi cha kutokuona ngozi basi inatosha kuosha juu yake
tu.
3.KUOSHA MIKONO HADI VIFUNDONI
kwa kuitikia kauli ya Mola Mtukufu :
“….NA
(osheni) MIKONO YENU MPAKA VIFUNDONI …” [5:6]
Imelazimu maji
yaenee vema katika nywele na ngozi.
Ukiwepo uchafu
chini ya kucha ukayazuiliya maji kupenya ndani au pete iliyobana isiyoruhusu
kupenya maji, udhu hautasihi bali utakuwa ni batili.
Imepokelewa na
Imam Muslim kwamba mtu mmoja alitawadha na akaacha (kuosha) sehemu ya kucha
mguuni. Mtume – Rehema na Amani zimshukie – akamuona na kumwambia :
“Rudi
ukatawadhe vizuri (kwa ukamilifu).
4. KUPAKAZA MAJI SEHEMU YA KICHWA
kwa kuitekeleza kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu :
“…NA MPAKE VICHWA VYENU …” [5:6]
Mapendeleo ya kupakaza maji ni kuupitisha mkono
uliorowa maji kichwani.
Na namna ya kupakaza ni kama ilivyothibiti katika
hadithi sahihi iliyopokelewa na Abdallah ibn Zayd kwamba Mtume – Rehema na
Amani zimshukie – alipakaza (maji) kichwa chake kwa mikono yake, akaipeleka
mbele halafu akairudisha nyuma.
Alianzia sehemu ya mbele ya kichwa chake kisha
akaipeleka kichogoni, kisha akairudisha pale mahala alipoanzia”
5. KUOSHA MGUU HADI VIFUNDON
kwa kulishika neno lake Mola
Mtukufu
“…NA (osheni)
MIGUU YENU MPAKA VIFUNDONI …”[5:6]
Inampasa mwenye kutawadha ahakikishe anaosha sehemu
yote iliyoainishwa katika sheria. Asiache sehemu yeyote ile iliyo chini ya
kucha.
Imepokelewa kutoka kwa Ibn Umar –Allah awawie Radhi –
amesema : Mtume wa Allah – Rehema na Amani zimshukie – alibakia nyuma yetu
safarini, kisha akatudiriki, tukaanza kutawadha na kupaka maji miguu yetu.
Mtume akalingana kwa sauti ya juu :
“Adhabu kali
ya moto itawathibitikia wenye kuacha kuosha visigino, (akasema hivyo) mara mbili
au tatu.
6. MPANGO/TARATIBU
Kutungamanisha baina ya viungo hivi vinne vya udhu kwa namna ilivyokuja
ndani ya Qur-ani Tukufu, ndiyo nguzo ya sita. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema :
“ENYI MLIOAMINI! MNAPOTAKA KUSWALI, BASI OSHENI NYUSO
ZENU NA MIKONO YENU MPAKA VIFUNDONI, NA MPAKE (maji) VICHWA VYENU, NA (osheni)
MIGUU YENU MPAKA VIFUNDONI” [5:6]
Utaratibu ndio mojawapo ya faida tunazozipata kutokana
na aya hii na pia utaratibu unapatikana kutokana na utendaji wake Bwana Mtume
kwani yeye hakutawadha ila kwa kuzitungamanisha nguzo, moja ikifuatiwa na
mwenziwe kama ilivyothibiti katika hadithi nyingi sahihi.
Kwa hivyo imempasa mwenye kutawadha mwenye kutawadha
aanze na kuosha uso, kisha aoshe mikono, halafu apakaze kichwa maji na amalizie
na kuosha miguu.
Mambo sita haya ndiyo yanayoitwa nguzo za udhu.
Kusihi ama kutokusihi kwa udhu wa mtu kunategemea sana utekelezaji wake.
Akiyatekeleza yote kama itakiwavyo udhu wake ni sahihi
na akiacha mojawapo ya mambo sita haya, udhu wake ni batili.
.
0 comments:
Post a Comment