NGUZO ZA SWALA, VITENDO VYA WAJIBU NA SUNNAH KATIKA
SWALAH
بسم الله الرحمن الرحيم
Nguzo za Swalah ni 14:
Nguzo ni zile ambazo
ukiswali na ukaziacha kwa makusudi Swalah yako inabatilika, na ikiwa umeacha
kwa kusahau, Swalah yako pia itakuwa haikukamilika hadi urejee kitendo chenyewe
au urejee rakaa na kisha mwishoni utoe Sajdatus-Sahw. Lakini ukiwa umesahau
nguzo ya Takbiyratul-Ihraam, basi itakubidi uiswali Swalah upya
tokea mwanzo.
Nguzo hizo 14 ni hizi
zifuatazo:
1. Kusimama
katika Swalah za Fardh kwa yule mwenye uwezo. (Wanachuoni wengine wamesema
nguzo ya kwanza ni Niyah kabla ya Kusimama). Allaah (Subhaanahu
wa Ta'ala) Anasema: "Na simameni kwa ajili ya Allaah hali ya kuwa watiifu" (Al-Baqarah: 238). Na Mtume (Swalla
Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Swali hali ya kuwa umesimama, usipoweza, basi kwa
kukaa na usipoweza basi kwa kulala ubavu" (Al-Bukhaariy na Abu Daawuud).
2. Takbira
ya kuhirimia (Takbiyratul-Ihraam) kwa tamko la Allaahu Akbar kutokana
na kauli ya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): "Ufunguo wa Swalah ni kujitwaharisha, na kuifunga
ni Takbira, na kuifungua ni kutoa Salaam" (Abu Daawuud na At-Tirmidhiy).
3. Kusoma
Suratul-Faatihah katika kila rakaa. Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi
wa aalihi wa sallam) anasema: "Hapana Swalah kwa ambaye hakusoma Suratul Faatihah" (Al-Bukhaariy).
4. Kurukuu.
5. Utulivu
(Twumaaniynah) katika Rukuu.
6. I'itidaal
(hapa inaingia na kunyanyuka kutoka katika Rukuu hadi anaponyooka mtu).
7. Utulivu
katika I'Itidaal.
8. Kusujudu.
9. Utulivu
katika kusujudu. Kutulia wakati wa kurukuu, kusujudu, kusimama, kukaa
baina ya Sijdah mbili kwa msemo wa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi
wa sallam): "Kisha rukuu mpaka
utulizane hali ya kurukuu, kisha nyanyuka mpaka ulingane sawa hali ya kusimama,
kisha sujudu mpaka utulizane na hali umesujudu, kisha nyanyuka mpaka utulizane
hali ya kuwa umekaa" (Al-Bukhaariy).
10. Kikao baina ya
Sijda mbili.
11. Utulivu katika
kikao baina ya Sijda mbili.
12. Tashahhud
ya mwisho.
13. Kikao katika
Tashahhud ya mwisho.
14. Salaam (Kutoa
Salaam) ya kwanza.
Utahakikisha
unafuatanisha yote hayo kama utaratibu ulivyopangika.
Waajib Za Swalah
Ni lile ambalo ni wajibu
kulifanya au kusema, inaondoka kwa kusahau na kulazimisha mwenye kuswali
kusujudu sijdah mbili za kusahau. Yeyote mwenye kuacha kwa kusudi Swalah
yake inabatilika ikiwa anajua uwajibu wake.
Istilahi hii inatumika
kwa madhehebu ya Hanafi na Hanbali ila ma-Hanafi hawaoni kuwa mwenye kuacha
wajibu kwa kusudi inabatilisha Swalah yake bali yeye amefanya madhambi
anayostahiki adhabu. Ama ma-Maaliki na ma-Shaafi'y hawana kigawanyo hichi cha
Waajib kwao ila wao wana nguzo na Sunnah kwa ujumla wake.
Ama hapa tutaweka yale
yaliyotajwa ambayo yanaelekea kuwa na nguvu zaidi.
Kwanza kabla hatujataja
mambo yenyewe, tunapaswa kujua kuwa mambo ya Waajib ni yale ambayo vilevile
atakapoacha mtu kwa makusudi hubatilika Swalah yake, na atakapoacha kwa kusahau
inamtosheleza yeye kusujudu Sijda mbili za kusahau 'Sujuudus-Sahw'.
Ama mambo ya Waajib
ambayo yametajwa katika kitabu cha 'Swahiyhu Fiqhus-Sunnah' kwa dalili mbalimbali
za Aayah na Hadiyth ni 9 kama yafuatayo:
1. Du'aa ya ufunguzi wa Swalah 'Du'aa
al-Istiftaah'.
2. Kusema 'A'udhu biLlaahi Minash-Shaytwaan
ar-Rajiym' kabla ya kusoma 'BismiLlaah ar-Ramaanir Rahiym' na 'Suratul-Faatihah'.
3. Kusema 'Aamiyn' baada ya
Suratul-Faatihah.
4. Takbiyrah za kuhama baina ya kitendo na kitendo.
5. Kusema 'Sami'aLlaahu liman hamidah'
6. Kusema 'Rabbana Lakal Hamdu' katika I'itidaal.
7. Kusema 'Subhaana Rabbiyal 'Adhwiym'
wakati wa kurukuu na kusema 'Subhaana Rabbiyal A'ala' wakati wa
kusujudu.
8. Tashahhud ya kwanza.
9. Kikao cha Tashahhud ya kwanza.
Wanachuoni wengine
wametaja mambo ya Waajib ni 8 kama yafuatayo:
1. Takbiyrah nyingine zote isiyo ile ya Ihraam.
2. Kusema 'Sami'aLlaahu liman hamidah'
kwa Imaam na mwenye kuswali peke.
3. Kusema 'Rabbana Lakal Hamdu'.
4. Kusema 'Subhaana Rabbiyal 'Adhwiym’ mara
moja kwenye kurukuu.
5. Kusema 'Subhaana Rabbiyal A'ala' kwenye
kusujudu.
6. Kusema 'Rabbi-Ghfir liy' kwenye kikao
baina ta Sijda mbili.
7. Tashahhud ya mwanzo.
8. Kikao katika Tashahhud ya mwanzo.
Hizi ndizo maarufu zaidi
kwa wanachuoni wengine.
Sunnah Za Swalah
Hizi ni kauli na vitendo
zinazopendeza kuletwa katika Swalah. Mwenye kufanya hayo hupata thawabu wala
Swalah haibatiliki kwa kuachwa hata kwa kusudi. Wala sijdah ya kusahau
hailetwi. Hapa tuna vigawanyo viwili vya Sunnah katika Swalah; Sunnah za kauli
na Sunnah za vitendo.
Sunnah Za Kauli
1. Kisomo baada ya al-Faatihah.
2. Dhikr nyinginezo katika Rukuu.
3. Dhikr baada ya kusimama kutoka katika Rukuu na
baada ya kusema ‘Rabbana Lakal Hamd’.
4. Dhikr nyinginezo katika Sujuud.
5. Du’aa baina ya Sijdah mbili.
6. Kumswalia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa
aalihi wa sallam) katika Tashahhud ya kwanza na ya pili.
7. Du’aa baada ya Tashahhud ya kwanza na ya pili.
8. Salaam ya pili.
9. Dhikr na du’aa mbalimbali baada ya Swalah.
Sunnah Za Vitendo
1. Kuweka Sutrah (kizuizi mbele ya sehemu
unayoswalia) katika Swalah.
2. Kunyanyua mikono wakati wa Takbiyratul
Ihraam, na wakati wa kurukuu na na wakayi wa kunyanyuka kwayo na wakati wa kuinuka
kutoka katika Tashahhud ya kwanza. Na kadhalika wakati
unapoinama na kuinuka.
3. Kuweka mkono wa kuume juu ya mkono wa kushoto
juu ya kifua unaposimama kuswali.
4. Kutazama mahali pa kusujudu.
5. Kulingana sawa mgongo unaporukuu na
kutonyanyua kichwa au kukiinamisha sana, na kuweka viganja kwenye magoti mawili
na huku umeviachanisha vidole vya mikono na kuachanisha viwiko visiguse mbavu
au tumbo lako.
6. Kuteremka katika Sijdah kwa mikono miwili
kabla ya magoti (Wengine huona kushuka kwa magoti kabla ya mikono).
7. Kuimakinisha paji la uso, pua na mikono
(viganja viwili) kwenye ardhi pamoja na kupanua mikono isiguse mbavu zako; kuwe
na uwazi wa kuweza kupita kinyama kidogo. Na viganja vyako viwe usawa wa mabega
au masikio wakati uko katika kusujudu na viwiko vikiwa vimenyanyuliwa juu na
vidole vya mikono vikiwa vinaelekea Qiblah. Matumbo ya vidole vya miguu yakiwa
ardhini visigino vikielekea juu na hali vidole vya miguu vikielekea Qiblah.
8. Kulilalisha guu la kushoto na kulisimamisha la
kulia wakati wa kikao baina Sijdah mbili.
9. Kurefusha kikao baina ya Sijdah mbili.
10. Kikao cha mapumziko baada ya kukamilisha
rakaa ya kwanza na ya tatu.
11. Kutegemea ardhi kwa mikono wakati mtu
anaponyanyuka kutoka kusujudu na kwenda kwenye rakaa nyingine.
12. Kukaa kikao cha Iftiraash (Kusimamisha
mguu wa kulia na kukalia mguu wa kushoto) katika Tashahhud ya mwanzo. Na kukaa
kikao cha Tawarruk (kusimamisha mguu wa kulia na kuipitisha
mguu wa kushoto chini ya muundi wa mguu wa kulia na huku kikalio chako kimekaa
juu ya ardhi).
13. Kuashiria kwa kidole cha shahada katika
Tashahhud kuanzia mwanzo hadi mwisho bila kukishusha na huku unasoma na
ukikitazama.
(Abu Maalik Kamaal
Saalim, Swahiyh Fiqhus Sunnah, Mj. 1).
Hata hivyo, Shaykh Abu
Bakar Jaabir al-Jazaairiy katika kitabu chake Minhaajul Muslim yeye
amegawanya Sunnah za Swalah katika mafungu mawili: Zilizotiliwa mkazo kama vile
Waajib na zisizotiliwa mkazo.
Sunnah Zilizotiliwa
Mkazo
1. Kusoma Surah au Aayah katika Qur-aan baada ya
Suratul Faatihah katika Swalah ya Asubuhi, rakaa mbili za mwanzo za Swalah ya
Adhuhuri, Alasiri, Maghrib na 'Ishaa.
2. Kusema ‘Sami'a Alaahu liman Hamidah’ wakati
wa kuitadili na kisha Rabbaana walakal Hamd, Subhaana
Rabiyal 'Adhiym wakati wa kurukuu, Subhaana Rabiyal A'alaa wakati
wa kusujudu.
3. Takbira ya kuhama.
4. Tashahhud ya kwanza na tamko lake.
5. Kusoma kwa uwazi katika Swalah ya kusoma kwa
uwazi na kusoma kwa siri katika Swalah ya kusoma kwa siri.
6. Kumswalia Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi
wa aalihi wa sallam) katika Tashahhud ya mwisho.
Sunnah Zisizotiliwa
Mkazo
1. Du'aa
ya ufunguzi.
2. Kusoma
A’udhubiLlaah.
3. Kunyanyua
mikono miwili mpaka usawa wa mabega.
4. Kusema
Aamiyn.
5. Kurefusha
kisomo katika Swalah ya Asubuhi na kupunguza katika Swalah ya Alasiri na Maghribi.
6. Namna
ya mkao, nayo ni kukalia mguu katika vikao vyote na kukalia tako katika kikao
cha mwisho. Mikao ni wa Iftiraash (kukalia tumbo la mguu wa kushoto na
kuunyoosha unyayo wa mguu wa kulia) na Tawarruk (kuweka tumbo la mguu wa
kushoto chini ya paja la kulia na kuweka kikalio ardhini na kunyoosha unyayo wa
mguu wa kulia).
7. Kuweka
mikono juu ya kifua, wa kulia juu ya wa kushoto.
8. Du'aa
katika Sijdah.
9. Du'aa
katika Tahiyyaatu.
10. Kuanzia kulia
kutoa salaam.
11. Kutoa salaam ya
upande wa kushoto.
Ingawa kuna ikhtiliaaf
ya hao wanachuoni, tunapenda kuwakumbushia Hadiyth ya Mtume (Swalla
Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliyesema:
"Swalini kama mlivyoniona nikiswali" (Al-Bukhaariy).
Kwa hivyo, ni juu yetu
kufanya juhudi kufuata yote aliyofanya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi
wa aalihi wa sallam) ili tuchume thawabu nyingi zaidi.
0 comments:
Post a Comment